Kama umekuwa unajikuta kwenye hali ambayo watu hawakupi umakini unaostahili, unajua ni jinsi gani unaumia.
Labda ni kwenye kazi yako, unafanya kazi ambayo ni nzuri sana, lakini watu hawaijali kama unavyoijali wewe.
Unakazana kuboresha biashara yako, kwa kutoa huduma bora sana kwa wateja wako, lakini bado wengi hawathamini kile unachofanya.
Wakati mwingine ni maisha yako binafsi, watu wanakuchukulia poa sana kiasi cha kuona kama hustahili hivi. Mnapanga kukutana na mtu muda fulani anakusubirisha kweli, na hata anapofika hachukulii uzito kwenye mkutano wenu.
Kama hayo yamekuchosha, kuna suluhisho bora kwako, suluhisho ambalo ni rahisi na unaweza kulifanyia kazi.
Suluhisho hilo ni hili, anza kujipa umakini wewe mwenyewe.
Kile ambacho unataka wengine wakithamini, anza kukithamini wewe mwenyewe.
Ni kazi yako, umeifanya kwa juhudi sana, umeweka thamani kubwa, halafu anakuja mtu na kuanza kuidharau, unakubaliana naye. Hapana, kataa, mwambie aache kabisa hiyo dharau kwa kazi yako na kama haitaki basi aende kwingine na siyo kudharau kazi yako.
Ni biashara yako, unakazana kutoa huduma bora kwa wateja wako, lakini anakuja mteja ambaye hathamini unachofanya, analeta dharau zake, usimwache aendelee kuleta dharau, mwambie aache na kama hawezi aondoke kwa sababu biashara haiwezi kumhudumia.
Mmepanga kukutana na mtu kwenye muda fulani, muda umefika lakini yeye hajafika, umeongeza muda zaidi hajafika, ondoka, usiendelee kumsubiri, hasa kama hajakupa sababu yoyote ya msingi. Akikuuliza kwa nini umeondoka mwambie unajali muda wako na una mengine yakufanya pia, kama yeye alivyokuwa na ya kufanya mpaka akachelewa.
Hizi ni hatua ngumu kuchukua, mwanzo utaona kuzichukua utaonekana una kiburi, lakini nakuhakikishia, utakapoanza kuchukua hatua hizi, utashangaa jinsi watu watakavyoanza kukupa umakini na heshima unayotaka. Wao wenyewe watabadili tabia zao kwa namna ambayo wataweza kwenda na wewe.
Anza kujipa umakini, na wengine watakupa umakini unaostahili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,