Tabia pekee ya sisi wanadamu ambayo imetupa mafanikio makubwa ni ushirikiano baina ya binadamu.

Katika ushirikiano huu, kuna kutoa na kupokea.

Kutoa ni sehemu ya ushirikiano huu ambayo inapewa uzito sana, kwa sababu ni rahisi watu kujisahau, wakapokea tu bila kutoa.

Hivyo ili kujenga jamii bora, lazima kila mtu awe na cha kutoa na cha kupokea pia.

Lakini kuna wakati kutoa kumekuwa kunatumika vibaya, kunatumika kama kisingizio cha mtu kukwepa majukumu ya kujijali yeye mwenyewe.

Sheria ya kwanza ya kutoa ni wewe kuwa na kile ambacho unakitoa, kama unataka kutoa ambacho wewe mwenyewe huna, jua hapo unakwenda kuwaumiza watu wawili, wewe mwenyewe na yule unayempa hicho unachotoa.

Unapotumia kusaidia wengine kama kivuli cha kukwepa majukumu yako, unageuka kuwa mwenye kuhitaji msaada zaidi ya yule unayemsaidia.

Upo mfano mmoja maarufu sana kwenye hili, unapokuwa kwenye ndege, unapewa maelekezo kwamba iwapo kutatokea ajali, basi unapaswa kujiwekea wewe kifaa cha kupata hewa ya oksijeni kabla hujamwekea mtu mwingine.

Hata kama upo na mtoto wako unayempenda sana, anza kuvaa kwanza wewe kabla hujamvalisha yeye. Sasa ukisema unaanza kumvalisha yeye kwa sababu unajali sana, wakati unahangaika kumvalisha, wewe unaishia oksijeni, unapoteza fahamu, sasa hapo mtoto hawezi kujivalisha mwenyewe na hawezi kukuvalisha wewe, kwa hiyo wote mnaishia kuumia na hata kufa.

Lakini kama wewe utavaa oksijeni kwanza, hata kama mtoto atazimia ukiwa unavaa, ukishavaa, ni rahisi kumvalisha na yeye na baada ya muda atazinduka.

Kila unaposukumwa kutoa, kumbuka sheria ya kwanza ya utoaji, hakikisha unakuwa na kile ambacho unataka kutoa.

Jisaidie wewe mwenyewe kwanza kabla hujakimbilia kumsaidia mtu mwingine, ili usije kutengeneza wahitaji msaada wawili.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha