Kila mtoto ana ndoto yake, mtoto yoyote ukimuuliza unataka kuwa nani hapo baadaye bila kujiuliza anakuambia mara moja. Watoto wanakuwa wanaamini kile wanachotaka huwa kinawezekana na wanakuwa hawana wasiwasi wowote juu ya kile anachokuambia.

Watoto wanaweza kufanya mambo makubwa sana kwa sababu ya imani yao ilivyokuwa kubwa. Mtoto mdogo ni rahisi kusimama na kusema ndoto yake bila hofu lakini mtoto huyo huyo akiwa mkubwa ukimuuliza aseme ndoto yake bila hofu anashindwa.

Mtoto mdogo kabisa anaweza hata akamshika nyoka na nyoka asimng’ate, lakini wewe mtu mzima ukimshika tu yule nyoka hawezi akakuacha salama. Lakini mtoto anakuwa hana hofu na hata nyoka anajua ni mtu salama kwake hawezi kumdhuru.

Image result for HO TO RISE TALENT OF THE KIDSImage result for HO TO RISE TALENT OF THE KIDS

Katika makala yetu ya leo tunakwenda kujifunza namna ya kukuza kipaji au ndoto ya mtoto wako. Najua kama una watoto huwa wanakuambia ndoto nyingi tu, hivyo leo utaondoka na maarifa ya kwenda kumsadia mtoto wako.

Hatua ya kwanza, mkutanishe na wale wanaoendana na ndoto ya mtoto wako. Kwa mfano, mtoto wako ndoto yake ni kuwa daktari bingwa wa moyo, jitahidi kumkutanisha na daktari anayeendana na ndoto yake.

Baada ya kumkutanisha mwachie mtoto ajielezee ndoto yake, awe huru kumuuliza maswali kwa mtu wake wa mfano.  Cha kufanya ni wewe kuongea na mtu huyo juu ya kile ambacho mtoto wako anataka ili aongee naye na kumpa hamasa kwenye kile anachotaka. Na vema kumkutanisha maeneo ya kazi, hata akimuona mavazi ya taaluma anayoitaka itamvutia zaidi.

Pia, mtu huyo wa mfano, muombe awe menta wa mtoto wako, kwenye kila hatua ya masomo yake awe anaongea naye, ampe msisitizo ni masomo gani anatakiwa awe vizuri ili aweze kufikia pale alipo. Angalau awe anaonana naye kama siyo kuonana ana kwa ana hata kuwasiliana naye kwa njia ya simu nayo inasaidia kumpa hamasa mtoto.

Hatua ya pili, mnunulie vitabu, kama umeona mtoto wako eneo fulani ndiyo analipenda, mtafutie vitabu vinavyoendana na kile anachopenda. Na bahati nzuri ni kwamba kwa sasa vitabu viko vingi, hakuna kile unachotaka kuwa ambaye wengine hawajafanya. Kupitia kusoma atajifunza vitu vingi zaidi ambavyo vitamsaidia kwenye kile anachokitaka.

Mtafutie kile anachotaka kuwa kwenye mtandao wa intaneti na akawa anajifunza kila anapohitaji.  Kwa sasa kila kitu unachotaka kipo kwenye mtandao wa intaneti ni wewe tu kuandika na kutafuta kile unachotaka kwa muda mfupi tu unakuwa umekipata tayari.

Pata muda maalumu wa kuongea naye juu ya ndoto yake. Usimwache akabaki bila kuwa na mwelekeo, wewe ndiyo mzazi wake ndiyo wa kumshika mkono.  Mtie moyo na mwaminishe kuwa utakua vile unavyotaka kuwa. Uwe mtu wa kumuonesha njia na siyo kumkatisha tamaa mtoto wako, kazi yako ni kumtia moyo, hata kama wewe ulishindwa usimwekee ugumu wowote mwache naye apambane na hali yake.

SOMA; Je Unataka Mtoto Wako Kusoma Shule Bora? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hapa

Unapokuwa unaongea naye hapo ndiyo muda mzuri wa kumuuliza maendeleo yake katika ndoto yake, masomo yake, anapitia changamoto gani na mengine mengi yanayoendana na hayo. Ukishamwandalia mtoto mazingira kama hayo ni lazima atakua kile anachokitaka kama akiwa katika mwongozo sahihi.

Jambo lingine ni mzazi kujiandaa kifedha, ndoto nyingine za watoto kuzifikia zinahitaji fedha nyingi kwa mfano, mtoto anataka kuwa rubani, usimkatishe tamaa kuwa sina fedha za kukusomesha kuwa rubani badala yake unatakiwa kuchukua hatua mapema sana na hatua hizo ni kama zifuatazo;

Unaweza ukafanya uwekezaji wa muda mrefu ambao kwa baadaye utakuja kumsaidia mtoto. Kwa mfano, kama ukinunua ekari nyingi za miti ukawa unazihudumia kwa miaka 10 ukija kuzivuna utakua umepata kiasi cha fedha ambacho kitamsaidia mtoto wako kutimiza ndoto yake.

Siyo lazima miti, bali uwekezaji wowote ambao utamsaidia kupata fedha za kutimiza ndoto za mtoto wako huu ni mfano tu.

Lakini pia, unaweza ukamfungulia akaunti za mfuko wa watoto yaani watoto fund kupitia uwekezaji wa UTT ambao unakuwa unamnunulia vipande na vinaendelea kujizalisha huku na wewe ukiendelea na mambo yako na mpaka utakapofika muda huo tayari utakua umepata kiasi cha fedha cha kumsomesha mtoto wako.

Hatua ya kuchukua leo; timiza ndoto ya mtoto wako kwa kumsaidia katika mwongozo uliojifunza leo.

Kwahiyo, utakapomwandalia mtoto mazingira mazuri ya kumpatia elimu bora utamsaidia sana. unatakiwa umsaidie mtoto kwa haki yake kwa kumpa elimu wezeshi. Hapo ni pamoja na kuhakikisha kiakili, kimwili  na kiroho yuko vizuri na wewe unakuwa vizuri maeneo hayo kwa pamoja mtafika mbali.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa http://kessydeo.home.blog ,vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana