Hakuna binadamu asiye na hofu,

Hofu ni sehemu yetu wanadamu, ndiyo kitu pekee kinachotufanya tuendelee kuwa hai.

Siku ambayo utaondoa kabisa hofu zote ulizonazo, ni siku ambayo utakuwa kwenye hatari kubwa.

Hofu ni njia ya akili zetu kutuambia tunapaswa kuwa makini zaidi na kitu kwa sababu kuna madhara makubwa mbeleni.

Pamoja na kwamba hofu ni sehemu yetu, wengi tumekuwa tunatumia hofu vibaya, tumekuwa tunaruhusu hofu iwe kikwazo kwetu kupiga hatua.

Hii ni kwa sababu tunaruhusu hofu kutawala fikra zetu kila wakati.

Dawa ya kuondokana na hili ni kutenga muda wa kuhofia.

Pale unapokuwa na jambo unalohofia, tenga muda mfupi ambapo utajiruhusu kuwa na hofu kuhusu jambo hilo. Fikiria kila baya linaloweza kutokea, jipe picha ya namna mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi.

Kisha muda huo unapoisha, rudi kwenye kuchukua hatua, chagua kile ambacho utafanya na peleka mawazo yako yote kwenye kitu hicho.

Muda wa kuhofia ukishapita, usiruhusu tena hofu ikae kwenye fikra zako. Hofu inapokunyemelea, andika pembeni kile unachohofia kisha jiambie kwenye wakati ujao wa kuhofia utakihofia utakavyo, ila kwa sasa, weka mawazo yako kwenye kile unachofanya.

Kwa kuchukua hatua hii, unajiweka kwenye nafasi ya kudhibiti fikra zako na kuweza kuchukua hatua. Watu kwa nje watakuona kama shujaa asiye na hofu, ila ndani yako unajua ni jinsi gani unaikabili hofu yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha