Mlipuko wa virusi vya Corona unaoendelea sasa duniani (COVID – 19) una madhara kwenye kila eneo la maisha yetu.

Madhara makubwa kabisa yako kwenye upande wa afya, siyo tu kwa mtu mmoja mmoja, bali kwa mfumo mzima wa afya. Kwa sababu uwezo wa mfumo huu ni mdogo ukilinganisha na uhitaji unaotokana na wengi wanaoambukizwa ugonjwa huu kwa haraka.

Madhara makubwa zaidi yapo kwenye uchumi, kwa sababu njia pekee ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu ni watu ambao hawajaambukizwa kujitenga (social distancing) na kwa wale wanaoumwa kuwekwa karantini.

Uchumi unategemea mzunguko, kama hakuna mzunguko wa watu, bidhaa na huduma, uchumi unayumba. Thamani ya fedha ipo kwenye mzunguko, haijalishi una fedha kiasi gani, kama huwezi kupata mahitaji yako, kutokana na biashara kufungwa, fedha hiyo inakosa thamani.

Kuyumba kwa uchumi kunakotokana na mlipuko huu wa Corona unaoendelea, unaathiri zaidi biashara ndogo na za kati kuliko biashara kubwa. Kwa madhara ya nje kama kupungua kwa wateja, kukosekana kwa malighafi au mali kunaweza kuathiri biashara zote kwa usawa. Lakini madhara ya ndani zaidi, kama kukosa wafanyakazi, kushindwa kurejesha madeni, yanaathiri zaidi biashara ndogo kuliko biashara kubwa.

Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza hatua za kila mfanyabiashara kuchukua wakati huu wa mlipuko, ili Corona isipelekee biashara yake kufa.

kunawa mikono.jpg

Kabla ya yote, hakikisha huogelei uchi.

Kabla hatujaingia kwenye hatua za kuchukua, nianze kwa kukuambia kwamba pamoja na ubaya wa changamoto hii, lakini pia ina manufaa yake.

Wakati wa changamoto kama hii, ndipo biashara bora na imara zinapojengwa.

Ukiangalia makampuni yote makubwa duniani, yalianzishwa au kuimarishwa wakati ambao kulikuwa na changamoto kubwa iliyoathiri uchumi.

Hivyo wewe kuwa kwenye biashara katika kipindi hiki, ni kitu kizuri, kwani utaweza kujua kama biashara unayofanya ni sahihi au la.

Majanga kama haya, huwa yanakuja kama ufagio au chujio, ambalo linatenga mchele na pumba.

Nikinukuu kauli ya mwekezaji Warren Buffett, amewahi kusema; “Only when the tide goes out do you discover who’s been swimming naked.”

Akimaanisha; ni mpaka pale mawimbi yanapotulia, ndiyo tunajua nani alikuwa anaogelea uchi.

Na hili liko wazi kabisa, mawimbi yanaficha mengi, huwezi kuona uhalisia wa watu wakati kuna mawimbi, hivyo waliovaa nguo za kuogelea na wanaoogelea uchi wote wanaonekana wanaogelea. Lakini wimbi linapotulia, mambo yanakuwa wazi, waliovaa nguo za kuogelea wanatofautishwa na wanaoogelea uchi.

Kwenye biashara, kuogelea uchi ni pale unapokuwa kwenye biashara isiyo na mchango wowote kwenye jamii, lakini kwa sababu mambo ni mazuri, unapata wateja wa kununua na hivyo kujiona upo kwenye biashara sahihi.

Lakini majanga kama haya yanapotokea, watu wanaacha kununua kwa matakwa yao na badala yake wananunua kwa mahitaji yao. Na hapo ndipo zile biashara ambazo hazina mchango wowote kwenye jamii na kwa watu zinakosa wateja na kufa.

Kwa maneno mengine, majanga kama haya ndiyo yanaonesha biashara ipi ina thamani kwa watu na ipi haina thamani. Biashara zenye thamani zinavuka majanga zikiwa imara, huku zisizo na thamani zikifa kutokana na majanga haya.

Swali la kujiuliza hapa ni je unaogelea uchi au umevaa nguo za kuogelea? Biashara yako inatoa thamani ambayo bado watu wanaihitaji licha ya kuwa kwenye changamoto kubwa au hakuna thamani unayotoa?

Hatua 10 za kuchukua kuzuia biashara yako isife kwa Virusi vya Corona.

Biashara yako haiwezi kuambukizwa virusi vya Corona, lakini mabadiliko ya tabia za watu kutokana na mlipuko huu yanaweza kupelekea biashara yako kufa. Ili kuizuia biashara yako isife kwenye mlipuko huu, chukua hatua hizi kumi.

MOJA; JUA THAMANI UNAYOTOA NA WAELEZE WATEJA WAKO.

Kama tulivyoona, biashara pekee zitakazovuka kipindi hiki salama ni zile ambazo zinatoa thamani kubwa kwa wateja wake na jamii kwa ujumla. Zile biashara ambazo watu hawawezi kuishi bila ya kuwa na kile kinachouzwa.

Hivyo huu ni wakati wa wewe kukaa chini na kujiuliza ni thamani gani unayoitoa kwa wateja wako. Huenda umezoea kuuza na kupokea fedha na umesahau thamani ipi unatoa.

Jiulize ni tatizo au hitaji gani la wateja ambalo biashara yako inatoa. Kisha waeleze wateja thamani hiyo vizuri, waoneshe jinsi ambavyo wanaihitaji thamani hii wakati huu wa mlipuko.

Mfano; biashara za huduma za kifedha zinatumia nafasi hii kuonesha jinsi ilivyo salama kutuma na kupokea fedha kwa mtandao na siyo fedha taslimu. Hii ni thamani kubwa ambayo mteja au mfanyabiashara hakuwa anaiona, lakini kwa sasa iko wazi.

MBILI; WAPE WATEJA WAKO MATUMAINI SAHIHI.

Wakati wa mlipuko kama huu, hakuna anayejua nini kitatokea kesho, na kadiri mambo yanavyozidi kuwa mabaya, ndivyo watu wanaendelea kutabiri kwamba mambo yatakuwa mabaya zaidi.

Watu wanatishana na kupeana wasiwasi mkubwa. Wapo wanaosema huu ndiyo mwisho wa dunia. Kila mtu ana maoni yake. Lakini tunajua kitu kimoja kuhusu maoni, siyo ukweli.

Hakuna aliyeweza kutabiri ujio au madhara ya mlipuko huu, na hakuna anayeweza kutabiri kwa uhakika mambo yataendaje. Tunachojua ni kwamba tutavuka hili, kama ambavyo jamii ya binadamu imevuka mengi siku za nyuma.

Hivyo wewe kuwa chanzo cha matumaini sahihi kwa wateja wako. Katika hali ya wasiwasi kama hii, watu wanapenda kuwasikiliza wale wanaoleta habari njema, lakini siyo habari njema hewa. Bali habari njema sahihi.

Usiwe mtu wa kutoa habari mbaya kwa wateja wako, utawatisha na kuwafanya waahirishe kununua. Badala yake kuwa mtu wa kutoa habari njema, mtu wa kuwapa wateja wako moyo na hapo watajisikia vizuri na kununua. Ukiweza kuwaonesha jinsi kile unachouza kinawasaidia kupunguza makali ya mlipuko, wateja wanakujali zaidi.

Mfano; biashara za ushauri na mafunzo zinapaswa kuwa chanzo cha matumaini kwa wateja wake. Kwa kuwaonesha kwamba hili linaloendelea siyo mwisho wa dunia na mambo yatakwenda vizuri baada ya hili.

TATU; BADILI MFUMO WA BIASHARA YAKO KUENDANA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA.

Maisha ya watu yamebadilika katika wakati huu wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Biashara yako pia inapaswa kubadilika ili kuweza kuwahudumia vizuri wateja wako.

Kama watu wanatumia muda mwingi nyumbani kuliko kutoka, usiendelee kusubiri wateja waje kwenye biashara yako, badala yake wafuate huko majumbani.

Badili mfumo wa biashara yako kutoka kusubiri wateja waje eneo la biashara na kufanya wateja waweze kuagiza wakiwa nyumbani na kupelekewa au kutumiwa kile walichoagiza.

Hatujui lini hali hii itaisha kwa hakika, hivyo usijiambie unasubiri mambo yatulie, badala yake chukua hatua sahihi ili uendelee kuwahudumia wateja wako.

Mfano; biashara ambazo zimekuwa zinategemea wateja waje kwenye biashara, ni wakati sahihi sasa kuweka mfumo wa wateja kuweza kuagiza wakiwa nyumbani na kisha kupelekewa au kutumiwa walichoagiza.

NNE; JIKINGE WEWE NA TIMU YAKO.

Wewe mfanyabiashara ukiumwa au wasaidizi wako wakiumwa, biashara itaathirika zaidi. Hivyo wewe na timu yako mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.

Hakikisha njia zote za kujikinga zinajulikana na kutumika na kila anayehusika kwenye biashara yako. Njia kuu zinafahamika, kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kushikana, kuepuka kushika uso. Hivi vyote vinapaswa kufanyiwa kazi.

Pia eneo la biashara liboreshwe kwa namna ambayo linapunguza maambukizi. Ukaribu baina yako au watoa huduma na wateja unapaswa kupunguzwa. Maeneo ya kunawa mikono yanapaswa kuwepo au dawa za kusafisha mikono kupatikana kwa urahisi.

Usiache kujilinda wewe na timu yako kwa kuepuka gharama, ukiugua wewe au timu yako, ni tiketi ya kifo kwa biashara yako.

Mfano; kwenye kila eneo la biashara kunapaswa kuwa na sehemu ya watu kunawa mikono kwa maji na sabuni au kwa dawa maalumu. Pia kama biashara inahusisha watu wengi, kuwekwe utaratibu wa kupunguza msongamano wakati huu. Kwenye huduma za afya, watoa huduma wanapaswa kuwa na vifaa vya ziada vya kujilinda wao wenyewe.

TANO; USITUMIE NAFASI HII KUNUFAIKA ZAIDI.

Katika hali ya mlipuko kama huu, ambapo watu hawana uhakika wa lini hali itarudi kama kawaida, wanakimbilia kufanya manunuzi makubwa. Hapa mfanyabiashara unapata tamaa ya kuongeza bei kwa sababu uhitaji ni mkubwa. Watu wanaweza kununua kwa bei juu kwa sababu hawana namna.

Lakini tambua kwamba huu mlipuko utapita, na kama unataka biashara yako iendelee kuwepo na iwe na wateja waaminifu hata baada ya mlipuko huu, usiutumie kujinufaisha zaidi.

Usiongeze bei kwa sababu tu kila mtu anaongeza bei na uhitaji ni mkubwa. Kama ulikuwa na mzigo wa kutosha kabla ya janga hili kuanza, endelea kuuza kwa bei zile zile. Na kama uhitaji ni mkubwa, wape kipaumbele wale wateja ambao umekuwa nao kwa muda mrefu.

Kama mlipuko umepelekea gharama za wewe kupata unachouza kuwa juu, waeleze wazi wateja wako kuhusu mabadiliko hayo. Usikimbilie tu kupandisha bei, jua wateja hawatasahau hilo na watavunja uaminifu kwenye biashara yako baada ya janga hili kupita.

Mfano; wauzaji wa vitu muhimu kama dawa, vifaa vya kujikinga, vyakula na vitu vingine wamekuwa wanapandisha bei katika nyakati kama hizi, wewe usifanye hivyo.

SITA; TOA ELIMU NA USHAURI SAHIHI KWA WATEJA WAKO.

Kwenye mlipuko unaoendelea sasa, kila mtu ni mwalimu, mshauri na mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko. Hata mtu ambaye mwezi mmoja uliopita alikuwa hajui (na huenda mpaka sasa) hajui kwamba kirusi siyo kiumbe hai kamili, ni mshauri mzuri sana kwa wengine kuhusu mlipuko unaoendelea.

Wewe wape wateja wako elimu sahihi, ambayo umeitoa kwenye vyanzo sahihi. Usilete ujuaji wako au kukusanya taarifa za mtandaoni na kufikiri hiyo ni elimu. Nenda kwenye vyanzo vya uhakika, na kwa hili la Corona, sikiliza taarifa za serikali na tembelea tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa anuani www.who.int kupata elimu sahihi kuhusu mlipuko huu wa Corona.

Mfano; kuna vitu vingi ambavyo watu wanashauriana kufanya, ambavyo siyo sahihi. Kwenye tovuti ya WHO, kuna kipengele wanakiita MYTH BUSTERS ambapo wanatoa ukweli kuhusu vitu visivyo sahihi wanavyoshauriana watu. Kama ulaji wa vitunguu hauzuii maambukizi ya Corona. Ingia kwenye tovuti hiyo, pata taarifa sahihi na kisha washauri wateja wako kwa usahihi.

SABA; JIHAKIKISHIE UPATIKANAJI WA MALI NA/AU MALIGHAFI.

Kama unafanya biashara ya kununua kwa jumla na kuuza kwa reja reja, unapaswa kujihakikishia upatikanaji wa mali katika kipindi hiki cha mlipuko. Kutokana na mipaka ya nchi nyingi kufungwa na shughuli kusimamishwa, hili linaathiri sana uzalishaji. Hivyo jipange mapema kwa kuhakikisha una mzigo wa kutosha katika kipindi cha mlipuko.

Kama unafanya biashara ya kuzalisha bidhaa, basi jihakikishie upatikanaji wa malighafi katika wakati huu wa mlipuko. Mabadiliko yanayoendelea yataathiri sana upatikanaji wa malighafi, jipange kwa kuhakikisha hilo haliathiri uzalishaji wako.

Mfano; wafanyabiashara wa bidhaa zinazotoka nje, kama nguo kutoka china, wamejikuta katika wakati mgumu kupata mzigo mpya tangu mlipuko huu uanze. Hivyo ni muhimu kuangalia njia nyingine ya kupata mzigo na kuhakikisha unapata mzigo wa kutosha kwa sababu hujui mlipuko huu utaisha lini.

NANE; MIKAKATI YA UKUZAJI BIASHARA IENDELEE.

Wakati wa majanga kama haya, wengi huacha kufanyia kazi mikakati yao ya ukuzaji wa biashara. Kwa kuwa hali ya uchumi inakuwa siyo nzuri, wateja siyo wengi na waliopo hawanunui sana, wafanyabiashara huona hakuna haja ya kujisumbua, badala yake wanasubiri mpaka mambo yawe vizuri.

Kama tulivyoona mpaka sasa, hakuna mwenye uhakika mambo yatarudi sawa lini, inaweza kuwa kesho, wiki ijayo, mwezi ujao au mwaka ujao, hakuna ajuaye.

Hivyo wewe endelea na mikakati yako ya ukuzaji wa biashara kama vile hakuna mlipuko unaoendelea.

Endelea na mkakati wako wa masoko kwenye matangazo na hata kuwatembelea wateja kule walipo, mtaa kwa mtaa, ofisi kwa ofisi na nyumba kwa nyumba. Ila hakikisha unajikinga na kuikinga timu yako.

Endelea na mkakati wa mauzo kwa kuwashawishi wateja kununua na kununua zaidi ya walivyopanga kununua.

Endelea na mkakati wa utoaji wa huduma bora sana kwa wateja wako ili wanunue tena kwako na wawaambie watu wao wa karibu kununua

Mikakati hii inapaswa kufanyiwa kazi kila siku, iwe kuna majanga au hakuna. Hata kama huoni matokeo yake kwa haraka, usiache kufanya.

Mfano; mikakati ya masoko, mauzo na huduma kwa wateja kwenye kila biashara inapaswa kuendelea kama vile hakuna kilichobadilika, ila iendane na hali halisi ilivyo sasa.

TISA; WASAIDIE WATEJA WALIOKWAMA.

Huu ndiyo wakati mzuri kwako mfanyabiashara kuwaonesha wateja waaminifu kwako kwamba biashara yako inawajali, haiangalii tu kuingiza faida, bali inataka mteja aendelee kuwepo.

Kuna baadhi ya wateja wako watakuwa wamekwama kutokana na hali inavyoendelea, iwapo watakueleza kukwama kwao na ukawa na njia ya kuwasaidia, wafanya hivyo. Kwa sababu usipowasaidia na wao wakashindwa, basi biashara yako itakuwa imepoteza mteja moja kwa moja.

Mfano; kama kuna wateja umekuwa nao kwa muda mrefu na wamekuwa walipaji wazuri bila kusumbua, ila kipindi hiki wameshindwa kulipa kwa wakati, wape nafasi ya kuchelewa kulipa au kulipa kwa viwango tofauti na awali kama ipo ndani ya uwezo wako.

KUMI; JIANDAE KWA MABADILIKO MAKUBWA YANAYOKUJA.

Kuna watu wanasema kwamba ugonjwa huu wa Corona ni mwisho wa dunia. Hilo ni kweli, lakini siyo kwa wanavyomaanisha wao. Corona siyo mwisho wa dunia kwamba watu wote watakufa. Ila Corona ni mwisho wa dunia kwamba baada ya janga hili kupita, dunia mpya itazaliwa, kila kitu kitabadilika.

Hakuna chochote kitakachobaki kama kilivyokua kabla ya Corona. Kuanzia mfumo wa afya, mfumo wa uchumi, ushirikiano wa kimataifa, ufanyaji kazi wa watu na hata tabia za wateja.

Watu kufanyia kazi majumbani kutaongezeka, matumizi ya fedha za noti na sarafu yatapungua, tabia ya watu kunawa mikono itaendelea na mengine mengi ambayo yanasisitizwa sana kipindi hiki.

Hivyo angalia ni jinsi gani biashara yako inaathirika na yale yanayoendelea sasa, kisha usijipe moyo kwamba hali hii itapita na biashara zitarudi kawaida. Jua kwamba hii ndiyo kawaida mpya.

Iandae biashara yako kuendana na mabadiliko yaliyopo sasa na mengine makubwa zaidi yanayokuja. Kufanya biashara kwa ukawaida na mazoea kumefika ukomo. Huu ni wakati wa mabadiliko, hivyo badilika la sivyo utakufa.

Mfano; biashara ambazo zilikuwa zinasubiri wateja kwenda kununua, zinapaswa kubadilika na kuweka mfumo wa wateja kuagiza na kisha kupelekewa au kutumiwa.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo hatua 10 za kuchukua ili kuilinda biashara yako isife kutokana na mabadiliko yanayoletwa na ugonjwa wa Corona. Ukichukua hatua hizo kumi, utaacha kuogelea uchi, hivyo wimbi linapotulia, huathiriki. Fanyia kazi hatua hizi 10 na biashara yako itavuka kipindi hiki salama na kuwa imara zaidi baada ya janga hili kupita.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania