Kama unafanya biashara na hukutani na changamoto, kuna makosa unafanya. Lakini pia kama changamoto unazokutana nazo ni zile zile, yaani zinajirudia, pia kuna makosa unafanya. Tutapata ufafanuzi wa hili kwa kina kwenye makala hii.
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu, hakuna siku tutakayoamka na tuwe hatuna changamoto kabisa. Hivyo kutamani usiwe na changamoto kabisa ni kujidanganya, badala yake unapaswa kuwa imara kuweza kukabiliana na changamoto ya kila aina.
Kwenye makala hizi za ushauri wa changamoto inayokuzuia kufanikiwa, tunashirikishana changamoto na hatua mbalimbali za kuchukua ili kuvuka changamoto hizo zisiwe kikwazo.
Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto kwenye biashara unayoipenda. Kabla hatujaangalia hatua za kuchukua kwenye hali kama hiyo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kuhusu eneo hilo.
Mimi ni msafirishaji na nipo kwenye usafirishaji kwa zaidi ya miaka 10, nashukuru nina malengo nayo makubwa na nimepiga hatua kubwa, ila changamoto ninazo kutana nazo kila siku zinanirudisha nyuma najitahidi kuendana nazo sawa, ila napata dalili za kukata tamaa, ninakosa furaha. Binafsi ni kazi inayo tembea kwenye damu yangu, Naipenda. Je nifanyeje? – Seif H. S.
Kama alivyotushirikisha msomaji mwenzetu, yupo kwenye biashara anayoipenda, lakini changamoto ni nyingi mpaka inampelekea kukata tamaa.
Zifuatazo ni hatua za kuchukua katika kukabiliana na changamoto unazokutana nazo kwenye biashara unayoipenda ili usikate tamaa.
Moja; jua chanzo halisi cha changamoto.
Hatua ya kwanza ya kuweza kukabiliana na changamoto unazokutana nazo, ni kujua chanzo halisi cha changamoto. Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Watu wengi wanashindwa kutatua changamoto kwa sababu hawajui chanzo chake halisi.
Tunaweza kuzigawa changamoto za maisha kwenye makundi mawili.
Kundi la kwanza ni changamoto mpya, hizi ni ambazo umekutana nazo kwa mara ya kwanza. Changamoto hizi huwa ni za ukuaji, umejaribu kitu kipya na ukakutana na changamoto. Hapa unachopaswa kufanya ni kujifunza njia sahihi ya kufanya kitu hicho na kuitumia ili kuvuka changamoto hiyo.
Kundi la pili ni changamoto za mazoea, hizi ni ambazo umekuwa unakutana nazo mara kwa mara. Kila wakati changamoto hiyo hiyo inajirudia. Hizi ni changamoto za mazoea, changamoto ambazo zinazalishwa na uzembe fulani unaoendelea kwenye eneo hilo lenye changamoto.
Kuwa na changamoto mpya ni jambo zuri, kwa kuwa ni kiashiria kwamba unakua. Kuwa na changamoto za mazoea siyo jambo zuri, kwa kuwa ni kiashiria kuna uzembe.
Kaa chini na orodhesha changamoto zote kubwa zinazoikabilia biashara yako, kisha jiulize ni changamoto mpya au changamoto za kujirudia. Kama ni changamoto mpya jifunze njia sahihi ya kufanya kitu ili uondokane na changamoto hiyo.
Kama ni changamoto za mazoea hapo kunahitaji kazi kubwa zaidi. Kwanza kabisa lazima wewe mwenyewe ubadilike, changamoto hizo zimekuwa zinajirudia kwa sababu yako, hivyo kama hutabadilika, hazitaweza kuondoka.
Pili tengeneza mfumo sahihi wa uendeshaji wa biashara yako. Changamoto nyingi kwenye biashara zinatokana na kukosekana kwa mfumo. Na kitu chochote kisichokuwa na mfumo, kinageuka kuwa fujo.
Angalia changamoto ambazo zinakabili biashara nyingi, kukosekana kwa wateja, mauzo kuwa chini, kutokutengeneza faida, kukosa wafanyakazi wazuri, zote hizo ni kukosekana kwa mfumo mzuri. Kama hakuna mfumo mzuri wa kuajiri, wafanyakazi wataajiriwa kwa sababu tu wanataka kazi, au kwa sababu ni ndugu, na kitakachotokea ni majanga. Kama hakuna mfumo wa masoko na mauzo, ni vigumu kupata wateja wapya au kuwashawishi wateja kununua.
Angalia kila eneo lenye changamoto, kisha litengenezee mfumo wa jinsi mambo yatakavyokuwa yanafanywa kwenye eneo hilo na changamoto zitaondoka. Ukiendelea kufanya kama unavyofanya sasa, tegemea changamoto kuwa kubwa zaidi ya zilivyo sasa.
Kwa msaada zaidi wa jinsi ya kutengeneza mfumo wa kuendesha biashara yako, karibu kwenye programu ya PERSONAL COACHING kwa kutuma ujumbe kwenda wasap namba 0717396253.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Timu Bora Itakayokuwezesha Kufanikiwa Kwenye Biashara.
Mbili; kuwa na ndoto kubwa unayoiishi kila siku na piga hatua ndogo ndogo.
Mara nyingi changamoto zinakusonga kwa sababu hakuna unachoangalia bali changamoto hizo. Unajikuta umeingia ndani ya biashara na kuwa biashara yenyewe, kitu kinachokupa upofu na usione kitu kingine bali changamoto zinazokukabili.
Ili kuondokana na hali hiyo, unapaswa kuwa na ndoto kubwa sana kwenye biashara yako, kuwa na picha ya mafanikio makubwa unayotaka kuyafikia na kila wakati kuangalia picha hiyo.
Kila unapokabiliana na changamoto mbalimbali, na kuchukua hatua za kuzitatua, jikumbushe picha yako kubwa unayotaka kuifikia. Picha hiyo itakusukuma kupiga hatua zaidi na kukuzuia usikate tamaa kwa changamoto unazokutana nazo.
Unapotoa macho yako kwenye picha kubwa unayotaka kuifikia, changamoto yoyote unayokabiliana nayo itaonekana kama ndiyo mwisho wa kila kitu.
Pamoja na kuwa na ndoto kubwa, kila siku piga hatua kuelekea kwenye ndoto hiyo. Kila siku fanya kitu kinachokupeleka mbele zaidi na hatua unazopiga zinakupa moyo kwamba inawezekana.
Tatu; pima mafanikio yako kwa viwango vyako.
Kitu kikubwa kinachowakatisha wengi tamaa kwenye kile wanachofanya ni kulinganisha mafanikio yao na ya watu wengine. Unapoangalia wengine na kuona wanapiga hatua, huku wewe ukikabiliana na changamoto, unaweza kujiona kama wewe ni wa kushindwa.
Kuna vitu viwili muhimu sana vya kuelewa na kufanyia kazi hapa.
Moja; kila mtu anakabiliana na changamoto fulani kwenye biashara yako na maisha yake pia. Hata wale unaowaona kwa nje wanacheka, siyo kwamba kila kitu kipo sawa kwao. Hivyo usiwaangalie na kuona wao mambo yao yako vizuri na ni wewe tu unayekabiliana na changamoto. Jua kila mtu kuna changamoto anakabiliana nayo.
Mbili; mafanikio siyo mashindano, bali ni safari ya mtu binafsi, usilinganishe mafanikio yako na ya watu wengine, bali jipime kwa hatua unazopiga kuelekea kwenye lengo ulilojiwekea. Angalia aina ya maisha unayotaka kuishi na yaishi huku ukiacha wengine wakiyaishi maisha yao.
Nne; furahia mchakato na siyo kusubiri matokeo.
Kama unasubiri matokeo ya mwisho, kufikia lengo kubwa ndiyo ufurahie, utasubiri sana na huenda hutalifikia, maana utakata tamaa mapema. Unapaswa kufurahia mchakato na siyo kusubiri matokeo.
Kila hatua unayopiga kwenye maisha na biashara yako, hata kama ni ndogo kiasi gani, ifurahie. Kila siku unayoikamilisha, itafakari na jua ulichofanya vizuri, ulichokosea na cha kuboresha, na imalize siku hiyo kwa ukamilifu na kufurahia kile ulichofanya.
Mafanikio kwenye maisha hayatokei siku moja, bali yanatengenezwa kwa muda mrefu. Furahia kila hatua unayopiga na safari yako itakuwa na furaha wakati wote.
Hata pale unapokabiliana na changamoto, angalia kitu kizuri kwenye changamoto hiyo, angalia nini unajifunza angalia inakusukuma kuwa bora kiasi gani na angalia inakuonesha kipi usichokiona.
Kile unachofanya ndiyo kipo kwenye udhibiti wako, matokeo unayoyapata yako nje ya udhibiti wako. Hivyo kazana na hatua unazochukua na usisumbuke na matokeo. Chukua hatua zilizo sahihi na matokeo yatakuja au yasije, unachojua ni ukichukua hatua sahihi kwa muda mrefu, utafika kule unakotaka kufika.
SOMA; Hatua Nane Za Kutengeneza Biashara Inayokupa Uhuru Mkubwa Na Unayoweza Kuiuza.
Tano; usifanye kila kitu peke yako.
Kama kila kitu kwenye biashara kinakutegemea wewe mwenyewe, hata changamoto ndogo zitaonekana ni kubwa. Kadiri biashara inavyokua, ndivyo mambo ya kufanya yanavyokuwa mengi. Hivyo pia unahitaji watu utakaowaamini na kuwapa majukumu ya kutekeleza na changamoto za kukabiliana nazo.
Kuwa na watu wengine ambao wanakutana na changamoto kabla yako, inasaidia mzigo wote usiwe kwako. Na hata kama utashiriki kwenye changamoto hiyo, vichwa viwili ni bora kuliko kichwa kimoja kwenye kutatua changamoto.
Hivyo cha kufanya tafuta watu wazuri, wenye uwezo wa kufanya kazi na wenye uadilifu wa hali ya juu, kisha wape majukumu kwenye biashara yako. Hiyo itakupa wewe muda wa kuhangaika na mambo makubwa na yenye tija, kuliko kusumbuka na kila aina ya changamoto.
Sita; pambana usife leo.
Kuna changamoto za kibiashara ambazo zipo kabisa nje ya uwezo wako, labda ni hali ya uchumi au sera za nchi au hali ya mazingira. Kwa changamoto za aina hii, huna namna ya kuzitatua. Uzuri ni kwamba changamoto za aina hii huwa hazidumu milele, huwa zinakuja na kuondoka.
Hivyo unapogundua upo kwenye changamoto za aina hii, kazi yako ni moja, kuhakikisha unapamba ili biashara yako isife leo. Yaani kila siku ni sawa na kuzima moto, lengo ni kuzuia biashara isife huku ukisubiri kipindi hicho kigumu kipite na mambo yatakaporudi vizuri basi utaendelea na mipango ya ukuaji.
Biashara inapokuwa inapitia kipindi kigumu kinachosababishwa na yale yanayoendelea nje ya biashara yenyewe, ni wakati wa kufanya yale ya msingi pekee, yale yatakayohakikisha biashara hiyo inaendelea kuwa hai kwa siku zijazo.
Saba; boresha maeneo mengine ya maisha yako.
Watu wanaotafuta mlinganyo kwenye maisha huwa wanafikiri kuna maisha ya kawaida na maisha ya kazi au biashara. Ukweli ni kwamba maisha yako ni kitu kimoja, kinachotokea kwenye maisha yako ya kawaida kinaathiri kazi/biashara yako na kinachotokea kwenye kazi/biashara kinaathiri maisha yako ya kawaida.
Changamoto za maeneo mengine ya maisha, kama mahusiano, afya na mengine, zinaweza kuathiri biashara yako pia. Hivyo unapopambana kukuza biashara yako, hakikisha hayo maeneo mengine yako vizuri.
Boresha mahusiano yako, maana hayo yana mchango mkubwa sana kwenye utulivu wako.
Boresha pia afya yako, maana bila afya bora hutaweza kukabiliana na changamoto za biashara. Kwenye afya zingatia afya ya mwili, akili na roho, vyote unavihitaji ili kuweza kukabiliana na changamoto unazokutana nazo.
Umejifunza mambo muhimu ya kukabiliana na changamoto kwenye biashara unayoipenda na kuondokana na hali ya kukata tamaa. Weka mambo haya kwenye matendo na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye biashara yako, huku ukiwa na furaha na utulivu wakati wote.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania