Upo kwenye sherehe na wakati wa kupata chakula umefika.

Kuna sehemu mbili za kuchukua chakula, sehemu moja ina vyakula vya kawaida ambavyo kila mtu anavipenda na sehemu nyingine ina vyakula vya kipekee ambavyo wewe ndiyo unavitaka.

Uko na marafiki zako kwenye sherehe hiyo, mnaongea mengi na mna wakati mzuri. Sasa wakati wa kuunga foleni kwenye chakula unafika. Marafiki zako wote wanaunga foleni kwenye sehemu yenye chakula cha kawaida kinachopendwa na kila mtu.

Wewe unataka kupata chakula cha tofauti na cha kipekee, lakini pia hutaki kupitwa na mazungumzo ambayo mnayafanya na marafiki zako. Na mazungumzo hayo yanaendelea wakati wapo kwenye foleni ya chakula. Na foleni hiyo itachukua muda mrefu.

Swali ni je utajiunga na foleni ipi?

Utajiunga foleni ya marafiki zako, upate kuwa nao lakini ukose chakula unachotaka?

Au utajiunga na foleni ya chakula unachotaka na ukose kuwa na marafiki zako?

Huu ni mtihani na njia panda tunayokutana nayo kwenye safari ya mafanikio.

Safari ya mafanikio ina foleni mbili, moja ni ya wale wanaofanya vitu vya kawaida, ambavyo vinafanywa na watu wengi. Na nyingine ni ile ya wanaofanya vitu vya tofauti ambavyo vinafanywa na wachache sana.

Foleni yenye watu wengi ina raha, unazungukwa na wengi na kamwe hujikuti mpweke. Lakini haitakufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Foleni yenye watu wachache ina upweke na magumu mengi, kuna wakati utaona kama kila kitu kinaanguka mbele yako, kama umepotea hivi. Utajiona wewe ndiyo huna furaha na maisha, huku ukiwaangalia waliopo kwenye foleni ya wengi wanavyoyafurahia maisha, inaweza kukuumiza sana.

Wengi wanaoijaribu foleni ya wachache hawawezi kumudu ugumu wake, hasa wanapoona wale waliopo kwenye foleni ya wachache wakiwa wanayafurahia maisha. Hivyo huishia kurudi kwenye foleni ya wengi.

Swali langu kwako rafiki yangu, umejiunga foleni ipi? Kama ni foleni yenye wachache, ambapo unapitia magumu lakini hukati tamaa na kutamani foleni ya wengi, karibu tuendelee kupambana pamoja hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Na kama umejiunga foleni ya wengi, kwa sababu huwezi upweke wa foleni ya wachache, kila la kheri katika kuwa kawaida.

Uhakika tulionao ni huu, miaka kumi ijayo, aliyekuwa analia sasa atakuwa anacheka na aliyekuwa anacheka sasa atakuwa analia. Aliyekuwa kwenye foleni ya upweke atakuwa amefikia hatua ya kuzungukwa na wengi na aliyekuwa kwenye foleni ya wengi, atajikuta kwenye upweke.

Chagua kwa usahihi, kisha beba jukumu la kile ulichochagua. Usilalamikie upweke wakati umechagua foleni ya wachache, kabiliana nao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha