Mmoja wa wanasayansi wa mageuzi (evolution) alifikiria kwamba asili huwa inatengeneza vitu vyenye matumizi. Kama kitu kitatengenezwa halafu kisitumiwe, basi huwa kinapotea.
Kwa kufikiri huko, alikuja na dhana kwamba hapo zamani, nyoka walikuwa na miguu, ila kwa kuwa hawakuitumia miguu yao, basi ilipotea. Hakuwa sahihi kwenye nyoka, lakini alikuwa sahihi kwenye uwepo na matumizi ya vitu.
Ni kweli kwamba kila kitu ambacho kipo, asili ina kazi nacho. Kama kitu kipo na hakina kazi kwa asili, kinakosa nguvu na kadiri muda unavyokwenda, kinapotea.
Hivyo tunaweza kusema kwamba, asili haifanyi kazi ya bure. Asili ina bajeti, haitumii vibaya nguvu na muda uliopo, kwa sababu hivi ni vitu muhimu sana.
Kwa hiyo basi, wewe kuwepo hapa duniani na kuwa hai mpaka leo siyo bahati mbaya, ni kwa sababu una matumizi.
Wewe kuwa kwenye kazi au kuwa na biashara mpaka leo, siyo kwa kuwa unastahili zaidi ya wengine, ila ni kwa sababu una matumizi, una uhitaji fulani ambao asili na wengine wanataka kupata kutoka kwako.
Hapa ni sehemu nzuri sana kwako kuanzia unapoyafikiria mafanikio yako, una matumizi gani kwenye asili, ni thamani ipi unatoa kwa wengine, ni nini wengine wanategemea kutoka kwako?
Kwa upande wa pili ni wale wanaokuzunguka, usimdharau mtu yeyote, hata kama unamwona ni mjinga na mzembe kiasi gani, kama bado yuko hai, jua asili ina matumizi naye, na huenda kuna siku na wewe utakuwa na matumizi naye, kuna siku utamtegemea sana, yeye anaweza kuja kushikilia maamuzi ya kama uishi au ufe.
Jikumbushe kwamba asili haifanyi kazi ya bure na hili litakukumbusha mambo mawili, kujithamini na unyenyekevu. Unajithamini kwa sababu unajua una mchango fulani kwa asili na wengine. Na unakuwa mnyenyekevu kwa sababu unajua kila anayekuzunguka, kila kinachokuzunguka kina mchango wa kukufanya uwe bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,