Ukiangalia jinsi ambavyo watu wanaendesha maisha yao, unaweza kushawishika labda wamehakikishiwa hakuna kifo, wataishi milele.
Kwa sababu utawaona wakifanya mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye maisha yao, wakiyafanya kwa adabu na uaminifu kama vile ndiyo kitu muhimu zaidi kwao kufanya.
Utawakuta watu wanafanya kazi ambazo hawazipendi, kwa zaidi ya miaka kumi, wakijiambia kuna siku wataondoka kwenye kazi hizo, lakini siku hawaijui, hapa unaweza kufikiria nini kama siyo watu hawa wamejipa uhakika wa kuishi milele?
Unapowakuwa watu hawana maelewano, wana chuki au wivu dhidi ya kila mmoja, utafikiri watu hao wataishi milele, hivyo wale wanaowasumbua au wasioelewana nao watawabughudhi kwa kipindi kirefu. Laiti kama watu wangekua muda tulionao hapa duniani ni mfupi, hakuna ambaye angepoteza muda huo kwenye chuki, mabishano na hata wivu dhidi ya mtu mwingine. Kwa sababu siku siyo nyingi, wewe au yule ambaye unamchukia kuna mmoja wenu atakufa. Na chuki au wivu haviwezi kusaidia lolote hapo.
Na yale mambo ya kupoteza muda, pale mtu anapojiambia anapumzika baada ya kazi ya siku nzima, lakini ukiangalia hiyo siku nzima, hakuna kikubwa alichofanya. Mtu anapanga kabisa atafanya kitu fulani, muda wa kukifanya unafika, anajiambia hajawa tayari au kujiambia kipi anakosa, kisha anajiambia atafanya kesho au siku zijazo. Hapo utawezaje kukataa kwamba mtu huyu ana uhakika wa kuishi milele?
Rafiki, ni wakati sasa wa kuacha kujidanganya, utakufa, na kibaya zaidi hujui ni lini. Uhakika tulionao ni kwamba miaka 100 kutoka leo, kila anayesoma hapa atakuwa amekufa.
Unaweza kuchukulia ukweli huo kwa namna mbili,
Moja ni kukata tamaa, kuona hakuna haja ya kujisumbua au kujitesa, unapaswa kula maisha kwa wakati huu ulionao. Lakini nikuonye, ukipita njia hiyo, utakikaribisha kifo kabla ya muda wake.
Mbili ni kupata matumaini makubwa na msukumo wa kutokupoteza muda kwa jambo lolote lile. Kuichukulia kila siku kama siku ya mwisho, hivyo kutokuahirisha chochote ulichopanga kufanya. Kuhakikisha unaikamilisha kila siku, na unapopata siku nyingine unaichukulia kama nyongeza kwako, ambayo pia unaitumia kwa uaminifu mkubwa.
Hutaishi milele, hivyo ishi kwa ukamilifu leo, huenda ndiyo siku pekee uliyonayo kwenye maisha yako, usikubali kuipoteza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,