Kama ni mfuatiliaji wa mwili wako, utagundua kwamba ukishafanya jambo moja kwa muda, mwili unajifunza na kuendelea kufanya wewe mwenyewe.

Mfano kama umezoea kuamka muda fulani kila siku, mwanzoni kwa kutumia alamu, baadaye unakuwa na uwezo wa kuamka kwenye muda huo hata kama huna alamu. Mwili unakuwa umejifunza huo ni muda wa kuamka na unaamka bila hata ya kuambiwa uamke.

Kadhalika muda wa kujisaidia haja kubwa, kama umejiwekea utaratibu kila asubuhi unapata haja, unakuta ndivyo inavyokuwa kila siku. Siku ukabadili na kuanza kupata jioni, utashangaa asubuhi hupati tena bali jioni.

Miili yetu ina tabia ya kurahisisha yale ambayo tunayafanya mara kwa mara, hivyo muda unapofika, unakuwa tayari kwenye kufanya jambo hilo.

Sasa unaweza kutumia tabia hii ya mwili kwa manufaa yako, kwa kupangilia siku yako kwa namna ambayo inajirudia kila siku.

Kisha kuchagua masaa ya siku ambayo utafanya vitu fulani. Kwa kurudia hivyo, mwili wako unakariri na unakuwa tayari kwa jambo hilo katika muda huo.

Mfano kuwa na muda ambao unaamka kila siku, na uwe muda huo huo kila siku. Ukifanya hivi kwa muda, mwili wako unazoea kuamka kwenye muda huo, baadaye haiwi kazi tena kwako kuamka.

Kuwa na muda ambao unalala kila siku, yaani ikifika saa fulani lazima ulale, hii inaufundisha mwili wako muda wa kupumzika, lakini pia inafanya muda wa kuamka ukifika uwe tayari kuamka bila ya usumbufu.

Tenga masaa mawili ya kwanza ya siku na yape kitu ambacho utakuwa unakifanya, kisha fanya kitu hicho kila siku. Iwe ni kuandika, kusoma,  au kazi zako nyingine, tenga muda huo na utumie kila siku bila kuacha hata siku moja. Mwili wako utajenga tabia kwamba muda fulani ni wa kufanya kitu fulani.

Tenga muda wako wa kufanya majukumu yako ya kazi, katika masaa hayo ni kazi tu. Mwili wako unajua kabisa kwamba muda fulani ni kazi na unajiandaa kwa hilo.

Tenga eneo ambalo utakuwa unafanyia kazi zako, na tumia eneo hilo kwa kazi tu. Unapofika kwenye eneo hilo, mwili wako unajiandaa kabisa kwa kazi.

Kazana sana kutengeneza utaratibu fulani ambao utaufuata kila siku, na mwili wako utakariri utaratibu huo kisha inakuwa rahisi kwako kuendelea kuufanya.

Usiwe mtu wa kuanza kila siku upya kama ndiyo siku ya kwanza ya maisha yako, wala usiruhusu usumbufu wowote kuingilia siku yako na kukuvuruga.

Pangilia muda wako wa kila siku na kuwa na nidhamu kubwa kwenye kufuata kile ulichopanga, kwa namna hii utaweza kufanya makubwa na kufanikiwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha