“Acquire worldly wisdom and adjust your behavior according. If your new behavior gives you a little temporary unpopularity with your peer group… then to hell with them.” – Charles T Munger
Charlie Munger hapa ana ushauri muhimu sana kuhusu maisha, ambao tukiufuata mambo yetu yatakuwa mazuri sana.
Anatuambia tunapaswa kupata hekima ya dunia na kisha kubadili tabia zetu kuendana na hekima hiyo.
Na iwapo tabia zetu mpya zinawafanya marafiki zetu wasituelewe, basi tunapaswa kuachana nao mara moja.
Hapa ndipo wengi wanapokwama na ndiyo maana wanajifunza mengi lakini hakuna hatua wanayopiga kwenye maisha yao.
Unajifunza njia bora ya kuwa na maisha bora, unajifunza tabia unazopaswa kuziishi na mambo unayopaswa kufanya.
Unatoka ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kuanza kufanya mambo hayo makubwa.
Lakini unaona uwaeleze rafiki zako kuhusu mpango wako mpya,
Na hapo wanaanza kukukosoa na kukukatisha tamaa,
Wanakuambia huwezi au haiwezekani,
Wanakuambia acha kujidanganya,
Wanakuonesha mifano ya wengine waliojaribu kufanya unachotaka kufanya na wakashindwa.
Na wewe kwa sababu unawapenda na kuwaamini sana marafiki zako, unaamini wako sahihi na hamasa uliyokuwa nayo inazima moja kwa moja na hakuna unachofanya.
Inatosha sasa, hupaswi tena kuendelea na utaratibu huo.
Hivi ndivyo utakavyofanya kuanzia sasa,
Utajifunza misingi na tabia sahihi kwako kuishi ili kufanikiwa,
Utachagua kile unachotaka kufanya,
Kisha utaanza kufanyia kazi mara moja bila ya kumuuliza yeyote.
Na pale marafiki zako watakapokuambia mbona siku hizi hatukuelewi, waeleze ni mpango gani ulionao na waambie wazi hutali maoni au ushauri wowote kwenye hilo.
Na hapo wape machaguo mawili, wakuelewe kwa namna hiyo na kuendelee kuwa pamoja au wasikuelewe na urafiki uishie hapo hapo.
Inahitaji msimamo mkali sana kuweza kufanya hivi,
Na ndiyo maana ni watu wachache mno wanaopata kile wanachotaka.
Wengine wengi wanakazana kuwafurahisha wengine,
Usiwe mmoja wao.
Jifunze hekima ya dunia na badili tabia zako ziendane na kile ulichojifunza na kama kuna ambao hawatayaelewa mabadiliko yako, achana nao.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania