“If you accept the obstacle and work with what you’re given, an alternative will present itself—another piece of what you’re trying to assemble.” – Marcus Aurelius
Watu wengi huwa wana mipango mikubwa kwenye maisha yao.
Lakini wanapoanza kufanyia kazi mipango hiyo, vikwazo na changamoto mbalimbali huwa zinaibuka.
Hapo ndipo wengi hukata tamaa na kuona walichopanga hakiwezekani tena.
Hapo wanachagua kuacha na unakuwa ndiyo mwisho wao.
Usikubali kuendelea na hali hii, ya kukata tamaa unapokutana na vikwazo.
Kwa sababu vikwazo ndiyo njia ya kukufikisha kule unakotaka kufika.
Vikwazo vinakuwa njia pale unapovipokea na kuvifanyia kazi.
Hapo vinakufungulia njia mbadala ya kukufikisha kule unakotaka kufika.
Kwa sasa dunia nzima inapitia changamoto kubwa ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Kwa wengi hiki ni kikwazo na kimeshawapa sababu kwa nini hawawezi kufanya walichopanga.
Kuna watu wamekuwa wanaweka malengo fulani kila mwaka lakini hawayafanyii kazi, halafu mwaka huu 2020 watajiambia hawajaweza kufanyia kazi malengo yao kwa sababu ya Corona.
Wanasahau miaka mingine hakukuwa na Corona, lakini hawakutekeleza malengo na mipango yao.
Huu ni mwaka mzuri wa kuitumia Corona ambayo kwa wengi ni kikwazo kuwa njia kwako kufika kule unakotaka.
Labda Corona inekuja kukuonesha kwamba kazi unayoifanya siyo salama kama ulivyofikiri.
Labda imekuwa kukuonesha biashara unayofanya siyo ya uhakika kama ulivyofhani.
Au imekuja kukuonesha kwamba unahangaika na mengi yasiyo muhimu, ya muhimu ni machache ambayo ukiyafanya vizuri matokeo ni makubwa.
Huenda pia imekuja kukuonesha umuhimu wa wewe kuwa na mifereji mingi ya kipato na kiacha kutegemea mfereji mmoja pekee.
Inawezekana pia Corona imekuja kuumbua uongo ambao umekuwa unajipa, kwamba huna muda wa kufanya vitu fulani, sasa muda unao na hufanyi.
Lakini pia Corona imekuja kukuonesha kwamba namna ulivyokuwa ukifanya kazi yako au kuendesha biashara zako siyo sahihi. Kwamba kuna namna bora zaidi ambayo haiwezi kuathiriwa na hali kama hizi.
Na mengine mengi.
Kitu muhimu kabisa kukitafakari leo ni Corona imekuja kukufundisha nini?
Corona kwako ni njia ya kuelekea wapi?
Usihofu, usikimbie, usikate tamaa, badala yake chukua hatua sahihi sasa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania