Mafanikio yetu yanategemea sana ushirikiano wa watu wengine.
Lakini watu hao tunaotegemea kushirikiana nao, wamekuwa ndiyo chanzo kikuu cha changamoto kwetu.
Malalamiko juu ya wengine yamekuwa mengi.
Wafanyabiashara wanawalalamikia wateja wao, kwa sababu hawaielewi thamani wanayoitoa na wanataka kwa bei rahisi kuliko wao wanavyouza.
Waajiri wanawalalamikia wafanyakazi waliowaajiri kwa sababu hawajitumi kama wanavyotegemea wajitume.
Walio kwenye biashara za ubia wanawalalamikia wabia wenzao kwa sababu hawatekelezi kile walichoahidiana wakati wanaingia kwenye ubia.
Na hata wanandoa wanawalalamikia wenza wao kwa sababu wamebadilika baada ya kuingia kwenye ndoa.
Unaweza kulalamika utakavyo juu ya watu unaohitaji kushirikiana nao lakini hawakupi ushirikiano uliotegemea.
Lakini hakuna malalamiko yoyote utakayotoa yatawabadilisha au kukusaidia wewe.
Kwa sababu wengi wala hawafanyi makusudi, bali ndivyo walivyo, kama walikuahidi tofauti walikudanganya tu ili uwaamini, ila unachoona sasa ndiyo asili yao. Na asili ni kitu kigumu sana kubadilika, mpaka mtu aamue mwenyewe na ni baada ya kupata maumivu makubwa yanayomsukuma abadilike.
Hivyo basi, njia pekee ya kuepuka hali hii ya kuja kuwalaumu wengine, ni kuanza na watu sahihi. Anza na watu wenye asili na tabia ambazo zinanufaisha kile unachokitaka, na hapo hutalalamika tena.
Badala ya kuhangaika na kila mteja, chagua wateja ambao wanaielewa thamani unayoitoa kisha wahudumie vizuri, hawa hawatakusumbua kwa bei.
Badala ya kuajiri kila anayetaka kazi au kila anayekubali kufanya kazi kwa bei rahisi, au kila unayemjua na hana kazi na hivyo kutaka kumsaidia, anza kwa kuajiri watu sahihi. Watu wenye uwezo wa kufanya kazi unayowapa, wanaojituma, walio tayari kujifunza zaidi na wabunifu. Ukishakuwa na watu wenye tabia hizi, hutalalamika tena kuhusu wafanyakazi.
Badala ya kuingia kwenye ubia na mtu kwa sababu mnajuana na hivyo kuamini mtaenda pamoja, kwanza jua sifa zake, jua uimara wake na mapungufu yake. Huwezi kujua hayo kwa kumuuliza, bali kwa kuchunguza mwenendo na tabia zake za nyuma, mahusiano yake na wengine na hali yake kifedha. Kisha ukishaona ni mtu mwenye tabia ambazo mnaendana, wekeni makubaliano kabisa mwanzo kabla hamjaanza, ambapo kila mtu anakuwa na majukumu yake. Pia wekeni mchakato wa kutatua au kusuluhisha pale mtakapofikia hatua ya kutokuelewana au kukubaliana. Ukizingatia haya mwanzoni, hutakuja kumlalamikia yeyote kwenye ubia.
Badala ya kuingia kwenye mahusiano ya kindoa na kila unayekutana naye na kukuambia kwamba anakupenda, chunguza kwanza tabia na asili yake. Angalia mtazamo wake kuhusu maisha, jua kuhusu familia yake, angalia mahusiano yake na watu wengine na ona kama ni mtu wa kufanya maamuzi yake mwenyewe au anashinikizwa na wengine. Angalia uaminifu wake kwenye vitu vidogo vidogo na changamoto ambazo amewahi kupitia na jinsi alivyozikabili. Hili litakuwezesha kumjua mtu vizuri na hilo litapunguza changamoto nyingi za baadaye.
Anza na watu sahihi na utapunguza sana malalamiko yako kwa wengine.
Siyo rahisi kupata watu sahihi kwa asilimia 100, lakini unapojiwekea vigezo ambavyo utaviangalia, utapata walio bora kuliko kutokuwa na vigezo kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,