Kubishana ni jambo la hovyo sana unaloweza kufanya kwenye maisha yako.

Kwa sababu linakupotezea nguvu na muda na hakuna manufaa yoyote unayoyapata kwenye kubishana.

Hata kama utashinda ubishani, hutakuwa umemshinda uliyebishana naye, maana atazidi kusimamia upande wake.

Hivyo basi, unapaswa kuepuka mabishano kwa namna yoyote ile uwezavyo kwa sababu hayatakunufaisha.

Njia bora ya kufanya hivyo ni kuchagua kuyaishi maisha yako na kuwaacha wengine waishi maisha yao. Usijione kama wewe ndiyo uko sahihi kuliko wengine. Na pale ambapo haiwezi kuwasaidia watu au haina umuhimu, fanya machaguo yako kuwa siri kwako.

Pale ambapo ukiweka mambo yako wazi yanakaribisha watu kukukosoa na kukuambia unakosea au hauko sahihi, usiweke wazi. Na pale watu wanapojua kuhusu machaguo yako na kukuambia umekosea au hauko sahihi wajibu wao wako sahihi. Usijitetee wala kujielezea kwa namna yoyote ile, hakuna atakayekuelewa.

Ukishajua nini unataka kwenye maisha yako, na ukishajua njia sahihi ya kukipata, kinachobaki ni wewe kuchukua hatua sahihi, mengine yote achana nayo. Utawaona wengine wakifanya kinyume kabisa na kutegemea kupata matokeo bora, usijisumbue nao. Watakuja wengi kukuambia unakosea, usibishane nao.

Na kuwa makini sana kwenye kutoa ushauri, kwanza usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba umshauri. Na mtu akija kwako kutaka ushauri, mtake akueleze kwa kina kile ambacho anataka umshauri kabla hujampa ushauri wako, elewa hali yake na kisha mshauri. Kama analeta ubishi basi achana naye, mwambie hivyo ndivyo ungefanya kama ungekuwa wewe na sababu za kwa nini ungefanya, kisha mwache achague mwenyewe anafanya nini.

Mtu akija kwako kuomba ushauri, ukamshauri kitu sahihi kufanya, halafu yeye akaenda kufanya tofauti na akashindwa, usianze kumwambia ameshindwa kwa sababu hajakusikiliza, wewe endelea na maisha yako. Kama akitaka ushauri na kuja tena kwako hapo ndiyo unaweza kumwuliza kwa nini alifanya tofauti.

Ogopa ubishi kama sumu, kwa sababu mkishafika hatua ya kubishana, hisia zinaingia katikati yenu na kila mtu anatetea upande wake kwa gharama yoyote ile.

Lakini pia hili lisikufanye ujione uko sahihi kuliko wote, badala yake kama kuna mtu anapingana na wewe angalia kama kuna kitu cha kujifunza, chunguza kwa makini upande anaosimama yeye, na kama kuna kitu ambacho ni sahihi kifanye. Usijipe ujuaji na kuona huwezi kufanya wanachosema wengine, kumbuka hufanyi kumfurahisha yeyote, bali unafanya kupata unachotaka. Hivyo kama kuna njia sahihi ya kufanya kile unachofanya, na imetolewa na mtu mwingine, usiikatae, itumie njia hiyo.

Kitu cha kuepuka ni ubishani wa kijinga wa kutaka kushinda na uonekane unajua zaidi. Wanaojua hawaonekani kwa kubishana, bali kwa matokeo wanayozalisha. Weka juhudi kuzalisha matokeo na kama kuna wanaokupinga, wacha matokeo unayozalisha yabishane nao, wakati wewe uko ‘bize’ kuzalisha matokeo zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha