Ukipatwa na hasira beba jembe na uende ukalime, hii ni moja ya kauli zilizozoeleka, lakini yenye maana kubwa sana, japo wengi huwa hawaioni na kuitumia.
Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia ambapo sehemu kubwa ya maisha yetu inaendeshwa na hisia tunazokuwa nazo.
Hisia hizi zinaweza kuwa chanya au hasi na zinaweza kuchochewa na kitu chochote kile bila hata ya sisi wenyewe kujua.
Mfano umetoka nyumbani, huna tatizo lolote, unafikiria mipango yako ya siku na unajiona ukiwa umeipangilia siku yako vizuri. Ghafla anatokea mtu na kukumwagia maji machafu, haijalishi kama amefanya hivyo kwa bahati mbaya au makusudi, siku yako haitakwenda tena kama ulivyopanga. Kwa siku nzima utakuwa unafikiria tukio hilo na litavuruga kila kitu.
Hapo hisia hasi za hasira zinakuwa zimekuingia, na kila ukijaribu kuziondoa ndiyo zinazidi kupamba moto. Kila unapojaribu kuzikandamiza, ndiyo zinapata nguvu zaidi.
Hivyo hatua sahihi ya kuchukua pale unapopatwa na hisia hasi, siyo kuzikandamiza, bali kuzitumia kwa namna ambayo ni bora zaidi na itakupa manufaa.
Badala ya kuruhusu hasira zikusukume kufanya mambo ambayo utayajutia, tumia hisia hizo kwa ukuaji wako binafsi. Ule msukumo wa kulipa kisasi unaoupata ndani yako, upeleke kwenye kujiboresha zaidi wewe mwenyewe. Kwa sababu hasira ina nguvu kubwa, ukipeleka nguvu hiyo kwenye maendeleo binafsi, itakusaidia sana.
Hisia za huzuni huwa tunazipata mara kwa mara, pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea, kwa kupata kile ambacho hatukutaka kupata, huwa tunapatwa na huzuni. Badala ya kuruhusu huzuni hiyo ipelekee wewe kuona maisha hayana maana, unapaswa kuitumia kujua maana na kusudi la maisha yako. Pale unapokosa kile unachotaka sana na kupata usichotaka, kunakupa nafasi ya kujua thamani ya kile unachotaka, hivyo unapokipata unakithamini na kukitumia vizuri.
Wasiwasi ni hisia nyingine hasi ambayo inaweza kukuzuia usifanye kitu kabisa. Hisia za wasiwasi zinakufanya uone chochote uone huna cha kufanya au chochote utakachofanya hakiwezi kubadili hali iliyopo. Lakini hizi ni hisia nzuri kutumia kukusukuma kufanya kilicho bora wakati wote. Kila unapojikuta ukiwa na wasiwasi, chagua kufanya kilicho sahihi, na kisha kifanye kwa ubora wa hali ya juu. Usikubali kukwama kwa kuwa hujui ufanye nini, fanya kilicho sahihi, mara zote. Na kwa kila hali unayopitia, kuna kilicho sahihi kufanya, hivyo fanya hicho.
Hakuna hisia hasi ambayo huwezi kuitumia kwa manufaa, muhimu ni kutambua wakati hisia hizo zinapokuingia na kisha kutumia nguvu yake kwa manufaa yako na siyo kuruhusu nguvu ya hisia hizo zikuharibu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,