Kabla ya kuja kwa mfumo rasmi wa elimu, yaani hii elimu ya darasani, elimu ilikuwa ikitolewa kwa mtu kufanya kazi chini ya mbobezi kwenye kile anachotaka kujifunza. Kuba baadhi ya taaluma mpaka sasa zipo hivyo.

Mfano ulipotaka kuwa fundi, basi ulifanya kazi chini ya fundi, ambaye tayari ana ujuzi mkubwa. Ulifanya kazi hiyo kwa miaka mingi, huku ukijifunza hatua kwa hatua. Ulianzia chini kabisa kwa kazi za kutumwa tumbwa, baadaye unaanza kupewa majukumu madogo madogo na kukua kwa namna hiyo.

Elimu hii ilichukua miaka mingi mpaka kukamilika na mwanafunzi kuwa mbobezi, lakini alijifunza mengi ambayo yalimsaidia kwenye kazi zake na hata maisha kwa ujumla.

Uhitaji wa haraka wa wafanyakazi uliua elimu hiyo na kuleta elimu ya darasani, ambayo kazi yake ni kufyatua wasomi kama mashine inayofyatua matofali. Haijalishi wanajua walichosomea, muhimu ni wafaulu mtihani na kupata cheti.

Sasa iwe ulipitia elimu rasmi na ukapata cheti, au kuna kitu umeamua kufanya kwenye maisha yako, unapaswa kuwa chini ya mtu mwingine. Mtu unayemkubali na kumwamini na ambaye utajiweka kwenye mikono yake ili akusaidie kuwa bora kwenye kitu hicho.

Unajiweka kwenye mikono yake kwa kuwa tayari kujifunza yale anayokufundisha, kusikiliza, kukosolewa na hata kusukumwa wakati mwingine. Hiyo yote ni kwa sababu anakutaka wewe uwe bora katika kile ambacho umechagua kufanya.

Unahitaji menta, ambaye tayari alishafanya kile ambacho unataka kufanya, na/au kocha ambaye anaijua misingi sahihi ya wewe kufika kule unakotaka kufika. Yule unayechagua kuwa chini yake, lazima uwe unamwamini kiasi cha kuwa tayari kufanya kile anachokutaka ufanye, bila ya kuweka mashaka. Kwa sababu unajua anafanya kwa nia moja tu, ya wewe kuwa bora na siyo kwa yeye kunufaika zaidi.

Kwa dunia tunayoishi sasa, dunia yenye kila aina ya kelele, dunia ambayo changamoto ni nyingi, usipokuwa na mtu wa kukuongoza, huwezi kupiga hatua. Kila siku utakuwa unachoka, lakini huoni hatua unazopiga.

Chagua sasa mtu ambaye utakuwa chini yake, mweleze wazi ni wapi unakotaka kufika, kisha mwamini na msikilize kwa kile anachokuongoza kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha