“Life is the constant approach to death; therefore, life can be bliss only when death does not seem to be an evil.”
“Your life is a small stretch of unlimited time. So have a good look at it, and make the best of it”
– Leo Tolstoy

Kwa hali tuliyonayo sasa ya mlipuko wa virusi vya Corona, watu wakiambiwa mkojo ni dawa watakunywa.
Watu wanafanya vitu vya hovyo sana, bila ya kujiuliza iwapo ni sahihi au la.
Kwa sababu tu kuna mtu kasema ni kitu kinachosaidia, basi watu wanafanya.
Yote hii ni kwa sababu maisha ni matamu, hakuna mtu anayetaka kufa.
Lakini kama wenye hekima walivyowahi kusema, kitu huwa na thamani pale unapokwenda kukikosa.
Unapokuwa na kitu kwa wingi, hukithamini, unaona kipo tu.
Lakini unapokuwa na hatari ya kukikosa kitu, ghafla thamani yake inakuwa kubwa.
Kabla ya Corona kila mtu aliona maisha yapo tu.
Baada ya Corona kila mtu anapambana kuokoa maisha yake.

Leo nataka nikukumbushe kitu kimoja rafiki yangu,
Kitu ambacho kitakufanya uone thamani ya maisha yako kila siku.
Siku ulipozaliwa, ndiyo siku uliyopewa adhabu kamili ya maisha yako,
Adhabu hiyo ni kifo.
Hivyo kila siku mpya unayoiona kwenye maisha yako, ni siku ambayo unakikaribia kifo chako.
Huenda ikawa leo au huenda ikawa kesho, hakuna ajuaye siku,
Lakini kila mmoja anajua siku itafika ambapo atayaacha maisha haya.
Ila kwa kuwa hatujui ni lini, huwa tunajisahaulisha, tunapotezea.
Rai yangu kwako leo ni uache kupotezea.
Kila siku ukabili ukweli kama ulivyo,
Kwamba umezidi kukikaribia kifo chako,
Hivyo basi, kila siku mpya unayoipata, iishi kama ndiyo siku yako ya mwisho,
Siyo kwa kunywa mikojo au chochote utakachoambiwa ni tiba au kinga,
Bali kwa kufanya kile kilicho sahihi,
Ambacho unajua unapaswa kukifanya.
Usiyachezee maisha yako leo, halafu siku unayokutana na hatari ya kifo ndiyo unataharuki.
Jikumbushe hatari ya kifo unatembea nayo tangu siku uliyozaliwa,
Na kadiri unavyoendelea kuziona siku mpya, ndivyo unavyojisogeza karibu zaidi na kifo chako.
Kama unakufa leo, kuna vitu vichache sana ambavyo ni muhimu kwako.
Vingi unavyokwenda kuhangaika navyo leo, vinakosa kabisa umuhimu kama ungejua leo ndiyo siku yako ya mwisho.
Sasa huhitaji kusubiri yeyote akuambie leo ni siku yako ya mwisho, anza kuishi hivyo wewe mwenyewe.
Maisha yako ni kipande kifupi ambacho kina mengi ya kifanya, kitumie vizuri.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania