Miaka kama 10 iliyopita, wakati nikiwa mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii, wakati huo ukiwa mtandao wa facebook, nilikuwa nimejiwekea utaratibu kwamba sikubali kupitwa na chochote. Hivyo kama jana nilifika sehemu fulani, leo nahakikisha napitia yote mpaka pale nilipoishia jana.

Kipindi cha mwanzo hilo lilikuwa rahisi, kwa sababu ulikuwa unaweza kuperuzi mpaka ukafika mwisho, yaani kukawa hakuna tena habari mpya ambayo hujaiona katika yale unayofuatilia. Lakini baadaye mitandao hii ikawa inabadilika, kiasi kwamba hata uperuzi kiasi gani, huwezi kufika mwisho.

Kila unapoperuzi unaona habari mpya na nzuri zaidi, ukiendelea ndiyo unaletewa nyingine nzuri zaidi. Na hivyo ndivyo mitandao hiyo inatufanya tuwe wateja na tegemezi, kuona kwamba tunapitwa hivyo kuendelea kuperuzi.

Ninachotaka kukuambia leo rafiki yangu ni hiki, kwa sasa tunaishi kwenye mafuriko ya taarifa na maarifa. Kama lengo lako ni kupata kila aina ya maarifa na taarifa, umeshashindwa. Kwa sababu wakati tu unasoma hapa, mamilioni ya watu wameshaandika vitu kwenye mitandao mbalimbali, mamilioni ya video mpya zimewekwa kwenye mitandao na mengine mengi.

Hivyo badala ya kutaka kushindana na mtandao wa intaneti, kutaka kuhakikisha hupitwi na chochote, chagua eneo lako unalopenda kulifuatilia, kisha fuatilia hilo.

Na hata katika eneo moja, bado kuna maarifa mengi yanayotolewa na watu wengi, ambapo pia huna muda wa kuweza kufuatilia yote. Hivyo chagua vyanzo vichache unavyoviamini na vifuatilie hivyo. Hapo unajipa nafasi ya kuelewa kwa kina kile unachoifunza kwa hao wachache na kisha kukiweka kwenye maisha yako ili yawe bora zaidi.

Na katika mafuriko haya ya maarifa tunayopitia sasa, ni muhimu sana uweke vipaumbele vyako vizuri. Kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa kitabu, kitabu kinakuwa kimebeba maarifa mengi na yaliyoelezewa kwa kina, hivyo unapokisoma kwa utulivu, unajifunza mengi. Kipaumbele cha pili ni makala zilizoandikwa kwa undani, hizi zinakuwa zimechambua kwa kina kitu kimoja kwa namna utakayoelewa na kuchukua hatua. Kipaumbele cha tatu ni video au sauti, hapa ni mafunzo yanayokuwa yamerekodiwa kwa mfumo huo, lakini siyo vitabu, njia hii ni nzuri kutumia hata unapokuwa unafanya vitu vingine. Na kipaumbele cha mwisho ni mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, instagram na mingine.

Fuata mtiririko huo wa vipaumbele, chagua vyanzo vyako sahihi tenga muda wa kujifunza, kuwa na muda wa kutafakari yale uliyojifunza, chagua hatua utakazochukua na kisha chukua hatua hizo. Hiyo ndiyo njia pekee ya kunufaika na mtandao wa intaneti. Lakini ukitaka kushindana nao, huwezi kushinda, na nguvu yote unayoweka kwenye mashindano hayo, unakuwa umeipoteza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha