Hakuna kitu chenye nguvu ya kujenga au kubomoa maisha yetu kama fikra na mtazamo ambao tunakuwa nao. Zile fikra ambazo unazipa nafasi na muda mrefu kwenye akili yako, ndiyo zinazoishia kuamua maisha yako yatakuwa ya aina gani.

Chanzo kikuu cha wengi kukosa furaha kwenye maisha ni fikra na mitazamo ambayo wanakuwa nayo.

Leo tutakwenda kuangalia vitu viwili ambavyo vina nguvu kubwa ya kuharibu maisha yako. Vitu hivyo ni majuto na wasiwasi.

Majuto yana nguvu ya kuondoa furaha kwenye mambo ambayo tayari yameshapita. Unapokuwa na majuto, unafanya yale yaliyopita kuonekana hakuna kizuri ulichofanya. Unaona kosa moja ulilofanya na kusahau mazuri mengi ambayo umefanya katika kipindi hicho hicho.

Wasiwasi unaondoa fursa kwenye kipindi kinachokuja. Kadiri unavyokuwa na wasiwasi sasa, ndivyo unavyojizuia kuchukua hatua ambazo zingekunufaisha zaidi baadaye. Wasiwasi unakufanya uone mabaya tu kwenye siku zijazo, wakati kuna nafasi kubwa ya kuwa na mazuri.

Madhara makubwa zaidi ya majuto na wasiwasi ni kwenye wakati uliopo, kwani vyote kwa pamoja vinakuibia nguvu yako, nguvu ambayo ungeitumia sasa kufanya makubwa, unakuwa umeipoteza kwenye majuto ya yale yaliyopita na wasiwasi wa yale yajayo, vitu ambavyo havina mchango wowote kwenye wakati ulionao sasa.

Amua sasa kutokupoteza muda na nguvu zako kwa kuepuka majuto na wasiwasi. Ukishafanya kitu, jifunze na ondoka na somo, majuto achana nayo kwa sababu hayatakusaidia. Na kuhusu yale yanayokuja, fanya maandalizi sahihi leo ambayo yatakusaidia kesho, wasiwasi unaokuwa nao leo, hautabadili chochote kuhusu kesho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha