Katika wakati huu ambao tunapitia changamoto kubwa, kila mmoja anahitaji mfumo bora wa kuendesha maisha yake.
Mfumo ambao hautakwamishwa na chochote kile.
Moja ya vitu vitakavyokusaidia sana kwenye kuziishi siku zako vizuri,
Ni kutengeneza utaratibu wa siku yako ambao utauishi kila siku.
Utaratibu huo unaitwa ROUTINE.
Hapa unapangilia jinsi ambavyo kila siku yako itakwenda, na kisha kufuata mpango huo.
Kwenye mpango wako weka kabisa ni muda gani utakaoamka na kulala kila siku.
Weka muda ambao utafanya kazi zako.
Weka muda utakaokula.
Na weka muda ambao utapumzika.
Weka muda utakaokuwa na wale wa karibu kwako.
Kisha kila siku fuata utaratibu huo.
Yaandae mazingira yako kwa namna ambavyo itakuwa rahisi kufanya kile ulichopanga badala ya mazingira hayo kuwa kikwazo.
Jizuie sana kuacha kufanya kile ulichopanga kwa sababu tu hujisikii kufanya.
Sasa tupo kwenye changamoto, ni sawa na tupo vitani.
Ukiwa vitani hupigani pale unapojisikia, bali unapigana pale unapokabiliwa na adui.
Adui tuliyenaye ametuzunguka kila wakati,
Hivyo kuruhusu uendeshe siku yako kwa kujisikia, ni kumpa adui ushindi wa mezani.
Pangilia utaratibu wa siku yako ambao utauishi kila siku,
Unapoamka cha kwanza pitia utaratibu wako wa siku, kisha panga yale utakayokwenda kufanya.
Na baada ya hapo, siku yako inaongozwa na yale uliyopanga, na siyo kwa hisia zako au za wengine.
Ukitengeneza utaratibu mzuri wa siku na kuuishi kila siku,
Inafika mahali mwili wako unakuwa umezoea kiasi kwamba huhitaji tena nguvu kufanya ulichopanga,
Muda na mazingira vikishakuwa sawa, unafanya.
Endesha siku zako kwa utaratibu maalumu kila siku (ROUTINE) na kwa pamoja tutaweza kuvuka changamoto hii tukiwa bora zaidi.
Kocha.