“Never listen to those who blame others and speak well about you.” – Leo Tolstoy

Kamwe usiwasikilize wale ambao wanawalalamikia wengine na kukusifia wewe.
Kwa sababu wanapoenda kwa wengine, wanakulalamikia wewe na kuwasifia hao wengine.
Kamwe usiongeze neno kwa wale wanaowalalamikia au kuwalaumu wengine,
Maana watakapoenda kukulalamikia kwao, wataongeza chumvi zaidi kwenye kile ulichosema.
Ni asili yetu binadamu kufurahia pale tunaposifiwa,
Lakini angalia kupenda huko sifa kusije kuwa kikwazo kwako kama inavyokuwa kwa wengi.
Ukikitana na hao wenge tabia ya kulalamikia wengine na kukusifu wewe,
Hakikisha unayafupisha mazungumzo uwezavyo kwa kutokuongeza chochote.
Sema asante na endelea na mambo yako, huku ukijua kabisa sifa za mtu huyo siyo sahihi, lakini usijisumbue naye.
Ukishaona mtu analaumu na kulalamikia wengine, jua yeye mwenyewe ana shida mahali, ila hataki kuikubali.
Na hivyo anakupanga wewe ili ukubali kuibeba shida yake.

Unaweza kuliona hili kwenye mahusiano mbalimbali, pale unapoanza mahusiano na mtu na akalaumu ambao amewahi kuwa na mahusiano nao huko nyuma na kukusifia wewe, jua tu kuna majanga yanakuja.
Lipo pia kwenye biashara, unapata mteja anayelaumu wafanyabiashara wengine na kukusifia wewe, baadaye anageuka kuwa mzigo kwako.
Kadhalika kwenye kazi, kuajiriwa na hata kuajiri, unapokutana na mwajiri au mwajiriwa anayelalamikia wengine na kukusifia wewe, huwa anaishia kuwa mzigo kwako.

Usijidanganye kwamba wewe ni bora kuliko hao wanaolalamikiwa,
Bali jua wazi unaandaliwa kwa magumu ambayo hao wanaolalamikiwa hawakuweza kuendelea nayo.
Hivyo na wewe jiandae kuchukua hatua sahihi na zenye manufaa kwako,
Bila ya kupewa upofu na sifa za mtu huyo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania