Kuna tatizo au changamoto ambayo unapitia, ndiyo, kila mtu kuna wakati anakuwa kwenye hali hiyo.

Lakini kwa asili yetu binadamu, huwa tunakimbilia kujiuliza maswali ambayo hayana msaada wowote kwenye tatizo tunalokuwa tunapitia.

Nini kimesababisha tatizo?

Kwa nini mimi tu ndiyo nipate tatizo hili?

Nani atakuwa amechangia mimi kupata tatizo hili?

Nani anayestahili lawama za mimi kuingia kwenye tatizo hili?

Ukiondoa swali la kwanza ambalo litakusaidia kujua chanzo cha tatizo, hayo maswali mengine ambayo huwa tunayapenda sana, hayana msaada wowote.

Kukazana kuyajibu ni kupoteza muda wako, ni usumbufu ambao unakuondoa kwenye hatua sahihi za kutatua tatizo lako.

Kitu muhimu sana unapojikuta kwenye tatizo ni mpango wako wa kuondoka kwenye tatizo hiyo. Unategemea kufanya nini ili kutoka hapo ulipo sasa? Hilo ndiyo swali muhimu unalopaswa kulijibu, ambalo litakuwa na msaada kwako.

Nani kafanya nini na nani wa kulaumu haitakusaidia. Nani anakuchukuliaje pia haina msaada kwako. Kitakachokusaidia ni mipango na utekelezaji wa kutoka pale ulipokwama sasa.

Na hata kama hujui ni namna gani utatoka pale ulipokwama, wewe anza kwa kuchagua hatua za kuchukua, hatua ambazo ni sahihi na anza kuzichukua . Ukiwa kwenye ufanyaji, ni rahisi kupata njia bora zaidi kuliko ukiwa hujafanya.

Wekeza rasilimali zako muhimu (muda na nguvu) kwenye kujikwamua hapo ulipokwama sasa na siyo kuhangaika na jinsi ulivyofika hapo au nani wa kulaumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha