“In the meantime, cling tooth and nail to the following rule: not to give in to adversity, not to trust prosperity, and always take full note of fortune’s habit of behaving just as she pleases.” — SENECA

Asili huwa ina tabia ya kutushtukiza kwa mambo mbalimbali.
Pale tunapofikiri mambo yetu yanakwenda vizuri, ndipo changamoto huanza kuibuka na hivyo kujionea wazi kwamba mambo siyo mazuri kama tunavyofikiri.
Pale tunapoona tuna afya imara ndipo magonjwa huibuka na kutuonesha udhaifu tulionao kiafya.
Pale tunapoamini tuna utajiri ambao unaweza kutatua kila kitu ndipo zinapokuja changamoto ambazo zinaonesha ukomo wa utajiri huo.
Tumekuwa tunajidanganya sana, na asili imekuwa inatucheka kwa jinsi tunavyojikweza kwa mambo ambayo yapo kabisa nje ya uwezo wetu.

Kanuni ya kwanza na muhimu kabisa ya kuwa na maisha tulivu ni kutokujidanganya.
Kujua wazi kwamba jambo lolote linaweza kutokea, na hasa lile ambalo hutegemei lotokee.
Tuache kujidanganya kwamba tunaudhibiti wa kila kitu,
Maana asili huwa inafanya mambo yake kwa namna yake yenyewe, na siyo kwa namna tunavyotaka sisi.
Usiamini sana kwenye vile ulivyonavyo, kwa sababu vitu vingi tulivyonavyo hatuna udhibiti navyo.
Hivyo tunaweza kuvipoteza muda wowote ule, bila hata ya kujua sababu ya kuvipoteza.

Na la muhimu zaidi, usikate tamaa pale unapopitia magumu au changamoto mbalimbali.
Badala yake endelea kupambana, endelea kuchukua hatua zilizo sahihi.
Hata kama huoni dalili za kuvuka unachopitia, usikate tamaa.
Endelea kupambana, na kama juhudi zako hazitasaidia, basi muda utatatua.
Lakini ukiwa mtu wa kukata tamaa haraka, hakuna kikubwa utakachoweza kufanya.

Jikumbushe ukweli huu; maisha ni mlolongo wa changamoto mbalimbali, ukitatua moja, unakaribisha nyingine. Hivyo usijidanganye kuna wakati mambo yatakuwa vizuri bila ya changamoto yoyote. Na muhimu zaidi, asili huwa inajiendesha kwa mipango yake yenyewe, na siyo kuangalia wewe unataka nini. Hivyo wakati unapofikiri kila kitu kipo vizuri, ndiyo wakati ambapo asili ina tabia ya kukuonesha siyo kweli.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania