Kila mara kuna makosa ambayo huwa tunarudia rudia kuyafanya, kwa sababu tunakosa ujasiri wa kuchukua hatua sahihi kuzuia makosa hayo yasitokee.

Na kikubwa kinachotufanya tukose ujasiri huo ni kwa sababu tunataka kuwaridhisha wengine, hatupendi kuwaona wakiumia, na mwishowe tunaumia sasa.

Leo tutajikumbusha maeneo ambayo ukiweka ujasiri, utaacha kufanya makosa na hata kuumia kwa sababu ya wengine.

Kama mtu anakuchukia, usijali, mpuuze, chukulia kama hayupo kabisa kwenye maisha yako. Kwa kufanya hivyo, chuki yake kwako wala haitakusumbua. Lakini umekuwa hufanyi hivi, umekuwa unakazana kuchukua hatua ili mtu huyo abadilike na kukupenda, akukubali, na hapo ndipo anapokuchukia zaidi na kukuumiza zaidi. Kuwa jasiri, puuza wote wanaokuchukia na usimbembeleze yeyote akupende kama haitoki ndani yake mwenyewe.

Kama watu wanakupa ushauri mbaya, usiusikilize, usiufanyie kazi, acha kabisa maongezi nao kwenye eneo hilo ambalo wanakupa ushauri mbaya. Na hapo utakuwa huru kufanya kile kilicho sahihi kwako. Lakini umekuwa hufanyi hivyo, umekuwa unasikiliza kila aina ya ushauri, na kwa sababu watu wamekuambia wana uzoefu, au wamekuzidi kitu fulani, basi wanataka usikilize ushauri wao, na usipousikiliza au kuufanyia kazi, wanakuambia umeshindwa kwa kuwa hujawasikiliza. Ondokana na huo woga, kataa ushauri ambao siyo mzuri kwako, hata kama unatolewa na mzazi wako.

Kama watu wanakuja kwako na utapeli, ukatae, usikubaliane nao, waeleze wazi kwamba hutaki. Hapo utaepuka kuingia kwenye mitego yao ambayo wamekuwa wanaitumia kuwanasa watu. Lakini umekuwa hufanyi hivyo, umekuwa unawasikiliza, na kujiambia labda hii ni tofauti na zile nyingine, unaingia, unapoteza. Kuwa jasiri, kama kuna harufu ya utapeli mweleze mtu wazi kwamba hutaki, na usimbembeleze kwamba nitafute baadaye au acha nikafikirie, unampa nafasi ya kuja kukulaghai zaidi, moja kwa moja mwambie hutaki au huhitaji. Ujasiri kama huo utakuokoa na mengi.

Kama watu wanakualika kwenye vikao au mikutano ambayo unajua utaenda kupoteza muda wako na hakuna manufaa yoyote, usiende, eleza wazi kwamba hutaweza kufika. Lakini umekuwa hufanyi hivyo, umekuwa unaogopa kuwaambia watu huwezi kuudhuria, hivyo unaenda, uliambiwa mkutano utaanza saa nane na kumalizika saa kumi, umefika saa nane, watu bado hawajafika, mpaka saa tisa ndiyo wachache wamefika, mkutano unaanza saa tisa na nusu, mpaka saa 12 bado mkutano unaendelea, unaisha saa mbili na hakuna chochote ulichonufaika nacho. Umepoteza masaa zaidi ya sita bure. Ungekuwa jasiri na kusema huwezi kuhudhuria, ungetumia masaa hayo sita kwa mambo mengine yenye tija kwako.

Umejionea hapa rafiki, kukosa ujasiri wa kuwakatalia watu, kumekuwa chanzo cha wewe kufanya makosa na hata kupoteza au kutapeliwa vitu mbalimbali. Hiyo yote ni kwa sababu unataka kuwaridhisha wengine huku wewe ukiwa hujijali.

Kuanzia sasa nakutaka uwe jasiri, weka maslahi yako mbele, anza kujijali wewe kabla hujajali wengine. Na kama kuna kitu wengine wanafanya au wanakitaka kutoka kwako na NDIYO kubwa haianzii ndani yako, kuwa jasiri na sema HAPANA. Na wala huna haja ya kueleza sababu, wewe sema tu HAPANA, HUWEZI AU HUTAKI.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha