“People strive in this world, not for those things which are truly good, but for the possession of many things which they can call their property.” – Leo Tolstoy

Maisha yetu wanadamu yamejawa na kila aina ya vikwazo na changamoto.
Kila wakati kuna kitu ambacho tunakabiliana nacho,
Kitu kinachotunyima usingizi,
Kitu kinachotaka tujisukume zaidi ya tulivyozoea.

Sasa kuna vitu vingi vinavyoweza kutusumbua kwenye maisha yetu,
Lakini watu wengi wamekuwa wanachagua kusumbuliwa na vitu ambavyo havina umuhimu wowote.
Mfano umeona mwenzako ana kitu fulani, na wewe ukajiambia lazima uwe na kitu hicho, huwezi kuachwa nyuma.
Hivyo unasumbuka kweli kupata kitu hicho,
Lakini sababu za kusumbuka huko ni kutaka tu uonekane au ulingane na wengine.
Kwa namna hii, unateseka kwa kitu kisichokuwa na umuhimu wowote,
Kwa sababu ukishapata kile ulichokiona kwa mwingine, utaona vingine vikubwa zaidi kwa wengine.
Hivyo maisha yako yote yanakuwa ya kuhangaika na kutaka kufanana na wengine.

Kitu muhimu ambacho kinastahili kukusumbua, kukutesa na kukuhangaisha, ni kusudi la maisha yako.
Kufikia yule mtu ambaye ulizaliwa kuwa na kutoa kile ambacho kipo ndani yako,
Hili ndiyo linapaswa kukusumbua wewe,
Kwa sababu kilitekeleza, kunakufanya wewe ukue zaidi, ujitambue zaidi na ufikie nafsi halisi kwako.
Kadiri unavyojitambua, ndivyo unavyoona fursa za kufanya zaidi.
Na kadiri unavyofanya zaidi, ndivyo wewe na wengine wananufaika zaidi.
Hata unapopata unachotaka, huoni utupu badala yake utele,
Na pale unapokosa, huoni kama ndiyo mwisho wa dunia, bali unaona ni njia ya kujifunza zaidi.

Chagua mateso yako vizuri,
Unataka uteseke kwa kuiga wengine,
Au uteseka kwa kukazana kuwa wewe?
Fanya uchaguzi wako na ishi uchaguzi huo kila siku.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania