Unapotafuta watu wa kushirikiana nao kwenye shughuli unazofanya, iwe ni watu wa kuajiri au kuingia nao ubia kwenye biashara, tumia vigezo hivi vitatu; maadili, uwezo na ujuzi.
Vigezo hivi ndiyo vitakusaidia kupata watu bora na sahihi ambao unaweza kwenda nao kwa muda mrefu na kila mmoja wenu akanufaika.
Lakini kitu muhimu ni kwamba, unapaswa kwenda na mtiririko huo,
Yaani unapaswa kuanza kwa kuangalia maadili ambayo mtu anayo, misingi yake ni nini. Maadili ni kile ambacho mtu anaamini na anasimamia, kile ambacho mtu yuko tayari kukipigania kwa gharama yoyote ile. Kama mtu ana maadili mazuri, utanufaika kwa kushirikiana naye, lakini kama maadili yake ni mabovu, haijalishi sifa nyingine alizonazo, maadili hayo mabaya yatakuumiza.
Baada ya mtu kuvuka kigezo cha maadili, sasa nenda kwenye uwezo. Unahitaji mtu ambaye ana uwezo mkubwa ndani yake, mtu ambaye anaweza kupanga mambo yake na kujisimamia katika kuyafanya, mtu ambaye anafikiri kwa akili yake na kuja na njia bora za kufanya kitu. Huhitaji mtu ambaye inabidi umweleze kila kitu anachopaswa kufanya, umsukume kila wakati kufanya anachopaswa kufanya.
Mtu akishavuka kigezo cha maadili na uwezo, sasa angalia ujuzi, hapa ni ile taaluma ambayo mtu anayo ambayo inamwezesha kufanya kitu fulani. Hapo unachagua yule ambaye anaweza kufanya kile unachotaka afanye, yaani ana ujuzi wa kukifanya.
Watu wengi wanapotafuta watu wa kushirikiana nao, wamekuwa wakiangalia ujuzi kwanza kabla ya vitu vingine, na hilo ndiyo limekuwa chanzo cha migogoro mingi. Unampata mtu ambaye kweli ana ujuzi (mara nyingi wa vvyeti) lakini hana maadili mazuri na pia hana uwezo wa kujisimamia mwenyewe. Hivyo kila wakati ni misuguano na watu wengine kwa kuwa wanapishana maadili na kushindwa au kuchelewa kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya kutokuwa na uwezo.
Uzuri wa ujuzi ni kwamba, yeyote anaweza kufundishwa, ila maadili na uwezo, ni vitu ambavyo mtu hawezi kufundishwa. Hivyo ni bora ukate mtu mwenye maadili mazuri na uwezo mkubwa lakini hana ujuzi na ukamfundisha, kuliko upate mtu mwenye ujuzi mkubwa, lakini hana maadili mazuri na uwezo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,