“The prerequisite of a good life is peace between people, and the major obstacle to peace is pride. A person should be humble, prepared to be falsely accused, ready for everything; only then can he bring peace into his relationships and into the lives of others.” – Leo Tolstoy

Hitaji kuu la maisha bora na tulivu ni amani na maelewano baina ya watu.
Huwezi kuwa na maisha bora kama huna maelewano na watu wengine.
Kukosekana kwa amani baina yako na wengine kunayafanya maisha yakose maana.
Kikwazo kikuu cha amani ni majivuno.
Pale mtu anapokuwa na majivuno hawezi kuelewana na watu wengine.
Hivyo mtu anapaswa kuwa mnyenyekevu, akiwa tayari kutuhumiwa kwa yasiyo sahihi.
Kuwa tayari kwa lolote ndiyo njia pekee ya kuleta amani kwenye mahusiano na maisha kwa ujumla.

Lazima ujue wewe siyo bora sana kuliko wengine na wala wengine siyo bora au dhaifu sana kuliko wewe.
Hivyo wapende na kuwaheshimu wengine kama unavyojipenda na kujiheshimu mwenyewe.
Wewe kupata ambacho wengine hawana haimaanishi unaweza sana kuliko wao.
Wakati mwingine ni swala la muda tu, huenda umetangulia na wao wanakuja.
Hivyo epuka sana majivuno, kuwa mnyenyekevu na kila mtu atafurahia uwepo wako kwenye maisha yake.
Epuka sana kujisifia kila wakati au kujionesha wewe ni bora kuliko wengine.
Hata kama watu hawakuambii, inafika mahali wanachoka kusikia mambo yako tu na jinsi gani wewe ni bora kuliko wao.
Na utakapokutana na changamoto fulani, watafurahia sana kwamba angalau na wewe umeshindwa kwenye jambo fulani.

Majivuno yanaibua chuki, wivu na kutokuelewana.
Unyenyekevu unaibua upendo, ushirikiano na kuelewana.
Zama tunazoishi sasa, zama za mitandao ya kijamii, zimempa kila mtu uwanja wa kuwa na majivuno, kwa kuonesha mitandaoni jinsi mambo yake ni mazuri kuliko ya wengine.
Epuka sana mtego huo wa kutumia mitandao ya kijamii kwa majivuno.
Kuwa mnyenyekevu na maisha yako yatakuwa ya amani na utulivu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania