Sumaku ni chuma ambayo imepitia mabadiliko yanayoifanya iweze kuvuta chuma nyingine zinazofanana nayo.

Weka plastiki karibu na sumaku na haiwezi kuvuta plastiki hiyo.

Lakini weka chuma na mara moja itavutwa.

Kuna somo kubwa hapa la kujifunza kuhusu maisha na mafanikio.

Kwanza kabisa unahitaji kuwa mtu ambaye anayavutia mafanikio kuja kwako. Na ili kufanya hivyo lazima uchague ni vitu vya aina gani unataka kuvutia na hapo ndipo unapohitaji kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Kama hujui unachotaka, huwezi kusa sumaku.

Mbili unahitaji kuwavutia watu na fursa sahihi kwako, ambao wanaendana na kile unachotaka. Hapo sasa ndipo sumaku inapovuta vyuma na kuachana na plastiki au vitu vingine. Hata plastiki iwe nzuri na inayoshawishi kiasi gani, sumaku haihangaiki nayo, kwa sababu haina zile sifa ambazo inaangalia kwenye kitu inachokivuta.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyafanya maisha yako pia, kuacha kukimbizana na kila mtu na kila kitu na badala yake kuchagua wale sahihi kwako na kukimbizana nao. Usiyumbishwe na mwonekano wa nje wa kitu, badala yake angalia sifa ya ndani inayokupatia kile unachotaka.

Sumaku hata ikitupwa jalalani, haisahau inachovutia, kinabaki kuwa chuma tu. Kadhalika nawe pia, haijalishi uko wapi, jua kile unachotaka na tumia hicho kuvuta watu na rasilimali sahihi kuja kwako huku ukiachana na yasiyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha