I’ve read about 80 books a year for the past 50 years. I come from cultural breeding. I don’t have a cellphone. When you spend all your time checking your cellphone messages, or updating your Facebook (of course I don’t have a Facebook page) then you don’t have any time for reading.” – Valclav Smil
Ni kisingizio cha kila mtu kwamba hana muda.
Hana muda wa kuanzisha biashara ya pembeni huku akiendelea na ajira.
Hana muda wa kukuza biashara yake zaidi.
Hana muda wa kujenga na kuboresha mahusiano yake.
Hana muda wa kusoma vitabu na kujifunza zaidi.
Zamani nilikuwa nawaonea huruma wale wanaosema hawana muda, na kujaribu kuangalia namna gani wanaweza kukabiliana na hali hiyo ya kukosa muda.
Ni mpaka pale nilipofuatilia wengi, na kukuta siyo kweli kwamba hawana muda, bali wamekuwa wanachezea muda ambao wanaupata.
Hivyo siku hizi mtu akiniambia hana muda, wala sibishani naye, najua tu ametafuta njia rahisi ya kujidanganya.
Kabla hujajiambia huna muda, hakikisha;
1. Hufuatilii habari ya aina yoyote ile, wala kuangalia tv au kusikiliza redio.
2. Haupo kwenye mtandao wowote ule wa kijamii.
3. Huna simu janja (smartphone)
4. Huli milo mitatu kwa siku.
5. Hulali zaidi ya masaa 8 kwa siku.
6. Hufuatilii mambo ya watu wengine.
7. Huna muda unaotumia kwenda na kurudi kwenye shughuli zako.
8. Huna starehe ya aina yoyote ile.
9. Huhudhurii vikao vyovyote vile.
10. Huhangaiki na mambo yasiyo na tija kwako.
Kama unafanya chochote kati ya hayo hapo juu, una muda mwingi mno kiasi kwamba umechagua kuupoteza.
Kila unapojiambia huna muda, pitia siku saba zilizopita na orodhesha kila ambacho umefanya kwenye kila dakika, usiache hata kimoja.
Kisha orodhesha malengo makubwa unayofanyia kazi.
Halafu angalia kila ulichofanya, kinachangiaje wewe kufikia malengo hayo.
Kama hakina mchango, huo muda uliotumia kufanya kitu hicho, umeupoteza, yaani ni sawa na umechukua fedha na kuzitupa kwenye shimo la choo, au kuzichoma moto kabisa.
Ukiacha kuhangaika na mambo yasiyokuwa na mchango kwenye malengo yako makubwa,
Utapata muda mwingi mno wa kufanya yale muhimu zaidi kwako.
Kama Seneca alivyowahi kusema, tatizo la muda siyo kwamba tunao kwa uhaba na hivyo kutokutosha, bali tunao mwingi sana kiasi kwamba tumeamua kuupoteza.
Hii ilikuwa kweli miaka elfu 2 iliyopita, lakini ni kweli zaidi leo.
Unatapanya muda wako kwenye mambo ya hovyo, kama kufuatilia habari au kuzurura mitandaoni, kama vile umeambiwa utaishi milele.
Anza leo kuwa bahili wa muda wako,
Anza kuhoji kila unachofanya na muda wako,
Na utaona jinsi ambavyo una muda mwingi kwenye siku yako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania