“You could leave life right now. Let that determine what you do and say and think.” – Marcus Aurelius

Jinsi tunavyoendesha maisha yetu, utadhani tunaishi milele, tunapanga mambo na kuyaahirisha kila wakati kama vile tumehakikishiwa huo muda tunaoendelea kuusogeza mbele tunao.
Jinsi tunavyochezea muda tulionao, kwa mambo yasiyo na umuhimu, unaweza kudhani tuna chemchem ya muda isiyo kauka.
Lakini tunajua wazi kwamba muda ni kitu chenye uhaba mkubwa kwetu,
Tunajua saa moja tuliyopoteza kuhangaika na mambo yasiyo muhimu ni saa moja tuliyopunguza kwenye maisha yetu.

Tunapaswa kuendelea kujikumbusha hili kila siku na kila wakati,
Kwamba unaweza kutengana na maishs muda wowote, na muda huo hujui ni lini.
Inaweza kuwa leo au kesho au siku zijazo.
Kujikumbusha hili kunakusaidia kufikiri, kusema na kutenda kwa usahihi.
Badala ya kusumbuka kufikiri mambo yaliyopita au yajayo, weka fikra zako kwenye mambo ya sasa, kile unachofanya sasa. Usisumbuke sana na yajayo, ambayo hujui kama utayakuta.
Kadhalika kwenye kusema, ongea yale yaliyo sahihi, ambapo hata ukiachana na maisha leo, uliyosema yanabaki kuwa alama kubwa.
Matendo pia ni kitu muhimu kuzingatia kwenye ufupi wa maisha yetu,
Tenda yale ambayo ni muhimu kwa wakati ulionao, chochote ulichopanga kufanya, pambana ukifanye kama ulivyopanga.
Usiwe mwepesi kuahirisha mambo unayopanga kufanya.

Tukianza kuuangalia muda kwa umakini wake, tukiacha kujidanganya kwenye muda tulionao hapa duniani, tutaona wazi jinsi muda huo ulivyo na thamani na hivyo tutaacha kuuchezea hovyo.
Jikumbushe hili kila wakati, unaweza kutengana na maisha muda wowote, hivyo fikra, maneno na matendo yako yawe sahihi kila wakati.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania