“There is only one real knowledge: that which helps us to be free. Every other type of knowledge is mere amusement.” — VISHNU PURANA, INDIAN WISDOM
Maarifa ya kweli na sahihi kwako ni yale yanayokusaidia uwe huru zaidi.
Mengine nje ya hapo ni ya kujiburudisha tu.
Lengo kuu ni kuwa huru kwenye maisha,
Hivyo ni wajibu wako kutafuta maarifa yanayokufikisha kwenye lengo hilo.
Kila wakati pambana kupata maarifa yanayokusaidia kuwa huru zaidi.
Kwa kuwa tunaishi kwenye zama za maarifa, maarifa yanayokupa uhuru ni hazina kubwa.
Chukua mfano wa watu wawili wanaofanya kazi sehemu moja.
Mmoja ana maarifa sahihi ya uwekezaji na anayafanyia kazi, kwa kuwekeza sehemu ya kipato chake.
Mwingine hajui chochote kuhusu uwekezaji, hivyo kipato chake anakitumia tu.
Baada ya muda, aliye na maarifa ya uwekezaji na anayafanyia kazi atakuwa amefikia uhuru wa kifedha,
Huku yule asiyekuwa na maarifa hayo akiwa kwenye utumwa mkubwa wa kifedha, akiwa na madeni makubwa.
Kinachowatofautisha watu hao ni maarifa waliyonayo.
Kama kuna mtu amepiga hatua kuliko wewe, yuko huru zaidi ya ulivyo wewe.
Jua kuna kitu kimoja tu kinachomtofautisha yeye na wewe,
Kitu hicho ni maarifa aliyonayo.
Jiulize nini anajua ambacho wewe hujui, kisha weka muda wako kwenye kujifunza kile anachojua na ufanyie kazi yale unayojifunza.
Baada ya muda na wewe utakuwa huru.
Kwa kuwa tupo kwenye mafuriko ya maarifa na taarifa,
Uhuru ni kipimo kizuri cha kuchagua maarifs yaliyo sahihi kwako.
Kabla hujaruhusu kupokea maarifa au taarifa fulani,
Jiulize je inakwenda kukufanya uwe huru zaidi ya ulivyo sasa?
Kama jibu ni ndiyo basi pata taarifa hiyo.
Kama jibu ni hapana basi achana nayo.
Kwa kigezo hiki, habari zote unaziweka pembeni, hakuna habari itakayokufanya uwe bora zaidi, sana sana itakuongezea msongo.
Kadhalika mitandao ya kijamii, hutakuwa huru kwa kuzurura kwenye mitandao hiyo kila siku.
Chagua maarifa yaliyo sahihi kwako, kisha yapate na yafanyie kazi mara moja.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania