Watu wengi hawaridhiki na pale walipo sasa,
Iwe ni kiasi cha kipato wanachotengeneza, kazi au biashara wanayofanya au eneo wanaloishi.
Wengi tuna ndoto kubwa zaidi ya pale tulipo sasa.
Lakini ukweli ni kwamba, huwezi kufika kokote unakotaka kufika bila kuanzia hapo ulipo sasa.
Kazi kubwa unayotaka kufikia, inaanzia kwenye kazi ndogo uliyonayo sasa.
Biashara kubwa unayotaka kuwa nayo, itatokana na biashara ndogo uliyonayo sasa.
Hivyo basi, hapo ulipo sasa, ndipo haswa unapopaswa kuwa.
Kwa kuwa ndiyo sehemu sahihi kwako kuwa, ambapo ukipatumia vizuri, utaweza kufika kule unakotaka kufika.
Hivyo basi, acha kudharau pale ulipo, ndiyo siyo unapotaka kuwa, lakini lazima upaheshimu na kupatumia vizuri kufika unakotaka kufika.
Kama hutaweza kuheshimu padogo ulipo sasa, siyo tu hutaweza kufika pakubwa, bali tabia hiyo itaendelea hata ukifika pakubwa na itapelekea wewe kushindwa hata ukiweza kufika pakubwa.
Paheshimu ulipo sasa na jiulize ni jinsi gani unaweza kupatumia kufika pakubwa zaidi unakotazamia kufikia, kisha chukua hatua sahihi katika kukamilisha hilo.
Kwa malengo makubwa uliyonayo, jiulize hapo ulipo sasa kunawezaje kukufikisha kwenye malengo hayo makubwa, jua hatua za kuchukua kila siku kwa hapo ulipo ili kufikia malengo makubwa na chukua hatua hizo kila siku bila kuchoka.
Nidhamu yako kwenye mambo madogo itazaa matunda makubwa na itakuwezesha kuwa na matunda hayo makubwa kwa muda mrefu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,