Mtu mmoja amewahi kusema niambie mambo unayofanya kila siku kwenye muda wako na nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani.

Kauli hiyo ina maana kubwa sana, kwa sababu kule ambapo unapeleka umakini wako, ndiyo kunakojenga maisha yako. Vitu vinavyochukua muda wako ndiyo vitu vinavyokujenga.

Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba umakini wetu una uhaba mkubwa. Umakini huo ambao umejengwa kwa muda na nguvu, una ukomo. Una masaa 24 tu kwa siku na huwezi kuongeza zaidi ya hapo.

Ina maana unapotoa muda kufanya kitu fulani, huwezi tena kutumia muda huo kufanya kitu kingine. Mfano unapotoa muda kufuatilia habari zisizo na manufaa kwako, ni muda ambao huwezi kuutumia kujifunza vitu vyenye tija kwako.

Kutokana na ukomo huo mkubwa tulionao kwenye umakini, inapaswa kuwa kitu ambacho tunakilinda sana. Lakini hivyo sivyo ilivyo kwa wengi. Wengi wanaruhusu umakini wao utawanyike kwenye mambo haya yasiyo na tija.

Ili uweze kuwa na maisha unayoyataka, kwanza weka vipaumbele vya yale muhimu kwako kufanya na kuzingatia katika kuyapata maisha hayo. Jua yale maeneo ambayo yana matokeo makubwa ukiweka umakini wako, kisha weka umakini kwenye maeneo hayo.

Kwa wote ambao wanataka mafanikio makubwa kwenye maisha, kuna maeneo muhimu sana ambayo unapaswa kuyapa umakini wako na kupuuza mengine yote.

Eneo la kwanza ni kwenye afya yako binafsi, hii ndiyo wewe, afya yako isipokuwa vizuri, hakuna chochote kinachokuwa na maana. Afya hapa inajumuisha mwili, akili na roho.

Eneo la pili ni mahusiano yako na wale ambao ni wa karibu kwako. Mahusiano haya yanapaswa kuwa bora na tulivu ili umakini wako usisumbuliwe na mambo yasiyo na tija.

Eneo la tatu ni kazi au biashara yako. Kile unachofanya, unapaswa kukazana kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kila wakati kazana kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa awali.

Eneo la nne ni jamii inayokuzunguka. Wale watu wanaokuzunguka kwenye maisha yako, ni watu ambao wana kila unachotaka. Hivyo unapaswa kujua ni jinsi gani ya kuwashawishi wakupe unachotaka, kwa wewe kuanza kuwapa kile wanachotaka.

Ukiweka umakini wako kwenye mambo haya, kwa kukazana kuwa bora kwenye kila eneo, utafanyika kuwa mtu mpya. Utaanza kuona matokeo bora na ya tofauti utakayoyapata kwenye kila eneo la maisha yako.

Kwa kila jambo unalotaka kufanya, kabla hujaanza kufanya, jiulize kwanza linachangiaje kwenye vipaumbele vyako. Kama lina mchango basi lifanye kwa kuweka umakini wako wote na kuzuia usumbufu. Kama halina mchango acha kulifanya, hata kama kila mtu anafanya.

Kuwa makini sana na wezi wa umakini wetu ambao wamesambaa kila mahali. Kila mtu anawinda umakini wako, anataka uangalie kitu chake, japo kinaweza kisiwe na umuhimu wowote kwako. Atakudanganya kwamba usipoangalia utapitwa. Hilo siyo kweli, hakuna kitakachokupita kama umeweka vipaumbele vyako sahihi. Lakini kama utahangaika na kila kitu kwa kufikiri hupitwi, hapo ndipo utakapopitwa kwa sababu vipaumbele vyako unaviacha nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha