“If you wish to improve, be content to appear clueless or stupid in extraneous matters.” — Epictetus

Uteja wa habari na mitandao ya kijamii huwa unatengenezwa na kitu kimoja, hofu ya kupitwa.
Unatembelea mitandao hiyo kila mara na kufuatilia kila habari kwa kuhofia usipofanya hivyo basi utapitwa.
Unahofia kuna mambo makubwa yatakayokuwa yanaendelea na wewe yatakupita kama hutafuatilia kila wakati.
Lakini kufuatilia huko kunagharimu sana umakini wako,
Unapoteza muda na nguvu ambazo ungezitumia vizuri zingekuwezesha kupiga hatua.

Ni wakati sasa wa wewe kufuata ushauri wa Epictetus ambaye anakuambia kama unataka kupiga hatua kwenye maisha yako, basi lazima uwe tayari kuonekana mjinga kwenye mambo yasiyo na umuhimu kwako.
Kwa kauli fupi, kubali kupitwa na yake yasiyo na tija kwako.
Yaani hata usiruhusu yakusumbue,
Peleka umakini wako kwenye yale muhimu tu kwako.
Mitandao ya kijamii na habari havistahili kuchukua muda wako.
Bali muda wako weka kwenye maendeleo yako binafsi, kazi au biashara yako na mahusiano yako.

Wala usihofie pale watu wanapokuambia, hujui hiki kinachoendelea, au kile…
Wewe unahitaji kujua yale yanayokuhusu na yenye tija kwako, yatakayokufikisha kule unakotaka kufika.
Habari na mitandao ya kijamii siyo vitu vyenya mchango kwako kwa namna yoyote ile.
Ni biashara za watu ambao wanatumia kila mbinu kukushawishi upeleke umakini wako huko.
Usikubali kutekwa kirahisi, makinika,
Usikubali kutawaliwa na hofu ya kupitwa, jisikie vizuri kabisa pale unapokuwa hujui mengi yanayoendelea, lakini unajua kwa kina kile unachofanya.

Ili upate kilicho bora, lazima uwe tayari kuachana na kilicho kizuri.
Habari na mitandao ya kijamii vinaweza kuonekana ni vizuri kwako, lakini kumbuka mafanikio yako ni bora zaidi.
Hivyo achana na hivyo vizuri ili uweze kupata kilicho bora.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu umakini wako, fungua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/05/2013

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,