Upo usemi baina ya wawekezaji kwamba ukiona mkurugenzi mkuu (CEO) wa kampuni anaongea sana kwenye vyombo vya habari, basi jua kuna tatizo kwenye kampuni hiyo. Kuna kitu hakipo sawa au mkurugenzi huyo hafanyi kazi yake vizuri.
Usemi huo una ukweli ambao ukiujua na kuutumia utakusaidia.
Ni kweli kwamba kelele na kazi huwa haviendi pamoja. Unaweza kuchagua kufanya kazi au ukachagua kupiga kelele, lakini siyo vyote kwa pamoja.
Mtu mmoja amewahi kusema, wale wanaoomba ushauri mara nyingi siyo wafanyaji, ni wapiga kelele tu. Wale wanaouliza kila mara biashara gani wafanye, au wapi wawekeze, au vitabu gani wasome, hao huwa siyo wafanyaji. Hata ukiwashauri, wengi huwa hawafanyii kazi ushauri huo, kwa sababu siyo wafanyaji. Mtu huyo aliendelea kusema, kama mtu anataka kufanya kitu kweli, atapata njia ya kufanya, bila hata ya kumuuliza yeyote.
Tukienda kwenye sababu nako ni kelele tupu, wale ambao siyo wafanyaji, huja na kila aina ya sababu kwa nini hawafanyi. Ambacho hawakiri wazi ni kwamba wamechagua sababu badala ya kufanya. Wao wanaona kuna kingine kimewazuia na wanakitumia kama sababu, lakini ukweli kinachowazuia ni wao kutumia sababu.
Mitandao ya kijamii imetoa nafasi kwa wengi kupiga kelele badala ya kupiga kazi. Hebu fikiria mtu anayetumia mitandao hiyo akiamini anakuza kazi yake, mfano mwandishi ambaye anaweka kazi kwenye mitandao ya kijamii ili awe na wafuasi wengi, na akishakuwa nao lazima ajumuike nao, kuchati nao, kujibu mambo mbalimbali. Unafikiri mwandishi huyu atapata wapi muda wa kuandika? Anakuwa amechagua kelele na kutelekeza kazi.
Chagua kuifanya kazi yako, au chagua kupiga kelele. Huwezi kufanya vyote viwili kwa pamoja. Kama unataka kuacha alama idumuyo, chagua kufanya kazi, lakini kama unataka kusikika kwa kelele ambazo baada ya muda zitapotea, chagua kelele.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha kwa somo zuri ambalo kwangu najifunza utulivu uliopo ndani yangu
LikeLike
Karibu Beatus
LikeLike