Kanuni muhimu kabisa ya uchumi ni hii, kadiri kitu kinavyopatikana kwa wingi na urahisi, ndivyo thamani yake inakuwa ndogo na watu kutokuwa tayari kulipa gharama kubwa kukipata.
Hii ndiyo kanuni unayopaswa kuendesha nayo maisha yako, kupima kila unachotaka kufanya ili kujua thamani yake.
Kama unachofanya kinafanywa na kila mtu, usitegemee kulipwa kiasi kikubwa na hata kufanikiwa pia.
Na uwezo wa kila mtu kufanya unatokana na urahisi na kufurahia kufanya. Kama kitu ni rahisi kufanya, kila mtu atafanya. Pia kama kitu kinafurahisha kufanya, basi kila mtu atakifanya.
Hii inafanya mafanikio yawe kinyume na viti hivyo, urahisi na raha ya kufanya. Kile kitakachokufikisha wewe kwenye mafanikio ni kile ambacho siyo rahisi kufanya au hakifurahishi kufanya.
Ni wachache ambao wako tayari kufanya kitu kigumu wakati kuna vitu rahisi wanaweza kufanya. Au kufanya kitu ambacho hakiwafurahishi, wakati vipo vingi vya kufurahisha vya kufanya.
Chukua mfano huu; una dakika 30 ambazo huna cha kufanya, uko na simu yako. Kwenye simu hiyo una vitabu na mitandao ya kijamii. Utafanya nini? Kusoma kitabu ni kitu kigumu na ambacho hakikupi raha ya haraka. Kuingia kwenye mitandao ya kijamii ni kitu rahisi na kinakupa raha ya haraka kwa kujua yanayoendelea. Ndiyo maana utajikuta unatembelea mitandao ya kijamii badala ya kusoma kitabu, japo muda ni ule ule.
Hili linazidi kutuonesha kwa nini mafanikio ni magumu na yanafikiwa na wachache, kwa sababu ni vigumu sana kuacha kilicho rahisi na chenye raha, na kufanya kilicho kigumu na kisicho na raha. Mafanikio ni vita kati ya kufanya kilicho rahisi kwako na kilicho kigumu.
Jikumbushe hili kila wakati kabla hujafanya chochote, kama kila mtu anakifanya, kama ni rahisi na kama kinakupa raha ya haraka. Kwa vigezo hivyo vitatu, unaweza kupima thamani ya kitu kabla hujakifanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,