Kwenye safari ya mafanikio hakuna jeshi la mtu mmoja, kwamba utafanikiwa kwa kujitegemea wewe peke yako ni kujidanganya.
Unahitaji ushirikiano wa watu wengine kwenye maeneo mbalimbali ndiyo uweze kufanikiwa.
Kama ni biashara unahitaji kuwa na wabia, unahitaji kuajiri wasaidizi na unahitaji kupata wateja watakaonunua kile unachouza. Lakini kabla hujafika kwa wateja, mbia unayeshirikiana naye na wasaidizi unaowaajiri unapaswa kuwachagua kwa umakini, maana hao wanaweza kuwa kikwazo kwako kufika kwa wateja.
Kadhalika kwenye maeneo mengine ya maisha, unahitaji watu wa kushirikiana nao.
Japokuwa watu wa kushirikiana nao unaweza kuwapata kwa urahisi, siyo wote ni sahihi. Cha kusikitisha ni kwamba wengi siyo sahihi, hata wale wanaoonekana wana uhitaji sana, huwa siyo sahihi.
Mfano kama unatafuta msaidizi wa kuajiri, wengi wataonekana wanahitaji kweli kupata nafasi hiyo, lakini ni wachache sana watakaokuwa sahihi kwenye nafasi hiyo.
Unahitaji kuwa na kigezo sahihi cha kuchagua watu utakaoshirikiana nao kwenye kile unachofanya. Hapa tunakwenda kujifunza kutoka kwa moja wa makocha wenye mafanikio ambaye alikuwa na vigezo vikali katika kuchagua wachezaji wake.
Tukiweza kutumia vigezo hivi, tutaweza kuchuja na kupata watu sahihi ambao tukishirikiana nao watakuwa na manufaa kwetu badala ya kuwa mzigo kwetu.
Unahitaji kuangalia uwezo binafsi wa mtu, na hapa unaangalia uwezo wake wa kiakili na utayari wake wa kujifunza zaidi. Mtu ambaye hana uwezo atakuwa mzigo kwako, hata kama ana uhitaji kiasi gani. Kadhalika asiyejifunza atakukwamisha.
Unahitaji mtu awe tayari kujituma kwenye kazi, mtu anayependa kazi yake na kuwa tayari kuifanya kwa juhudi kubwa. Kama mtu anachelewa kufika kazini na kuwahi kuondoka, kama kila wakati anatafuta sababu za kuepuka au kupunguza kazi, atakuwa mzigo kwako. Mafanikio yanahitaji kazi, unahitaji anayeweza kuweka kazi kweli.
Unahitaji mtu mwenye uadilifu wa hali ya juu, mtu ambaye anatekeleza kile alichoahidi, mtu ambaye anafanya jambo sahihi kila wakati, hata kama hakuna anayemuona. Mtu wa aina hiyo unaweza kumwamini na kumpa majukumu makubwa. Kama mtu hana uadilifu na akawa na sifa hizo mbili zilizotangulia, atakumaliza kabisa.
Unahitaji mtu ambaye ni mpambanaji na asiyekata tamaa. Mtu ambaye akikutana na ugumu hakimbii, bali anaangalia jinsi ya kuuvuka. Mtu ambaye hajiambii haiwezekani, bali anajiuliza inawezekanaje. Mtu ambaye akija kwako na tatizo, tayari ameshaanza kufikiria suluhisho. Ukimpata mtu wa aina hii, atakutia moyo hata pale mambo yanapokuwa magumu kwako.
Zaidi unahitaji mtu anayeweza kushirikiana na wengine, mtu ambaye anakuwa sehemu ya timu na kujua kwamba mchango wa wengine kwake na wake kwa wengine ni muhimu kwa mafanikio. Mtu asiyeweza kuendana na wengine atakuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa. Mtu asiyeweza kucheza kama timu anatuwa mzigo.
Sifa hizo ni muhimu mtu unayeshirikiana naye awe nazo kama unataka kufanikiwa.
Lakini kuna bendera nyekundu unapaswa kuziangalia, hizi ukiziona kwa watu jihadhari nao, usidanganyike wala kushawishika kwamba sifa zao nzuri zitaondoa changamoto hizo. Watu wenye tabia hizo huwa hawabadiliki haraka na huleta maumivu hata kama kuna manufaa wanakupa.
Bendera nyekundu ya kuangalia (tabia za kujitahadharisha nazo);
- Mtu anayeona anajua kila kitu na hakuna kipya cha kujifunza.
- Mtu ambaye ana majibu ya kila kitu, hata kama hajui anajifanya anajua.
- Mtu ambaye kila kikwazo kwenye maisha yake ana watu wa kuwalaumu lakini siyo yeye.
- Mtu ambaye ana malengo ya kufanikiwa haraka na kwa njia za mkato.
- Mtu ambaye yeye yuko sahihi kwenye kila jambo na wengine ndiyo wanaokosea.
Itakuchukua muda kuwapata watu sahihi wa kushirikiana nao, hivyo usiwe na haraka na fanya zoezi hilo la kutafuta watu sahihi kuwa endelevu kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,