“The person who speaks much will seldom fulfill all his words in his actions. A wise person is always wary lest his words surpass his actions.” — CHINESE WISDOM

Mtu anayeongea sana huwa siyo mfanyaji,
Ni vigumu sana mtu kuweza kutekeleza kila anachosema kama anasema sana.
Mtu mwenye hekima ni mwangalifu kwenye maneno yake, anajizuia asiongee sana ili asishindwe kutekeleza anayoongea.

Kuna pande mbili za kujifunza kwenye hili;
Upande wa kwanza usiwe muongeaji sana, ongea machache na yaliyo muhimu. Ahidi kile tu unachoweza kutekeleza.
Kama huna uhakika wa kuweza kutekeleza ni bora usiahidi. Watu watathamini ukifanya kile ambacho hukuahidi, kuliko ukiahidi halafu usifanye.
Kuwa bahili sana wa maneno yako na fanya neno lako liwe sheria, kwamba ukisema basi unafanya kama ulivyosema.
Hilo litakujengea uaminifu mkubwa kwa wengine.

Upande wa pili ni kuwa makini na wale wanaoongea sana,
Ukikutana na watu wa aina hii, jiwekee tahadhari,
Huwa ni watu wenye maneno mazuri kweli kweli, yenye ushawishi mkubwa.
Ukiwasikiliza unaweza kuamini kila kitu kitakwenda vizuri,
Lakini kwenye kutekeleza hutaona kitu, zaidi ya maneno kuendelea kuwa mengi.
Ukikutana na mtu anayeongea sana, anayeahidi mengi, kuwa na wasiwasi, jua ni nadra sana akaweza kutekeleza hayo yote.
Hivyo usiweke imani yako yote kwa mtu wa aina hiyo, hata kama utakubaliana naye, kuwa na njia mbadala ili asikukwamishe.

Kuongea ni rahisi, kila mtu anaweza kufanya hivyo, na wengi ni waongeaji.
Kufanya ni kugumu, ni wachache mno wako tayari kutekeleza kile walichoahidi.
Kuwa mmoja wa hao wachache na kuwa na tahadhari kwa walio wengi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu utumwa mpya na mbaya unaoendelea duniani, fungua; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/14/2022

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,