Hakuna mtu anayeshindwa kwenye mapambano yoyote wakati yuko kwenye ulingo wa pambano.
Mtu anakuwa ameanza pambano akiwa tayari ameshashindwa.
Kinachoenda kutokea kwenye pambano ni kukamilisha tu, lakini ushindi au kushindwa kulishatokea kabla.
Hebu fikiria mtu anayeenda kwenye pambano akiwa na njia mbadala. Timu inayoingia uwanjani ikiwa na matokeo mbadala, kwamba hata tukitoa sare hakuna shida.
Unapoingia kwenye pambano lolote lile ukiwa tayari kukubali matokeo mengine yoyote isipokuwa ushindi, tayari umeshashindwa. Unaweza kwenda kushinda kwa bahati, labda kama mpinzani wako atakuwa mzembe, lakini jua umeingia kwenye pambano ukiwa umeshindwa.
Unapoingia kwenye pambano kwa lengo la kwenda kulinda usipoteze, kitendo tu cha kufikiria kutokupoteza, tayari ni kukubali kupoteza.
Unachotaka wewe ni ushindi, na haupo tayari kupokea kingine isipokuwa ushindi unaotaka.
Unapoingia kwenye pambano lolote lile, jiambie wazi kauli hii ya kishujaa; sitakubali kuwa laini, kupunguza kasi, kunyamaza au kukata tamaa mpaka pale nitakapopata ninachotaka. Haijalishi mambo ni magumu kiasi gani, ndiyo kwanza nimeanza.
Kwa kauli hiyo umetangaza wazi kwamba unachotaka wewe ni ushindi, na siyo kingine. Haijalishi umeanguka mara ngapi, uko tayari kuinuka na kuendelea.
Vikwazo vingi vinavyokukwamisha vinaanzia kwenye akili, unaona kitu ni kikubwa kuliko uhalisia wake. Ukikiangalia kila kitu kwa uhalisia wake, na kusema hakuna namna kitakuwa kikwazo kwako, utashangaa jinsi vikwazo hivyo vinavyoyeyuka.
Lakini pia usijidanganye, usifikiri kwa kujiambia hakuli hii vikwazo vitakuogopa, usifikiri hutashindwa. Pale tu utakapotangaza kwamba unachotaka ni ushindi tu, hapo hapo utapata pigo moja kubwa la kutikisa imani yako. Ni kawaida ya asili kupima wale wenye matamanio makubwa, kutaka kujua kama kweli wakipewa matamanio yao wataweza kuyatunza na kunufaisha wengine au watayachezea.
Kama pigo utakalopata litakupoteza, asili inakuwa imejihakikishia kwamba usingefaa kupewa matamanio yako. Lakini kama utaendelea licha ya pigo hilo, asili itajua imepata mtu sahihi wa kumpa siri zake na uwezo wake mkubwa.
Kila ushindi unaoutaka unaanzia ndani yako, kwa kukata shauri kwamba unataka ushindi na kuwa tayari kuweka kazi ya uhakika kufikia ushindi huo. Huku ukiwa tayari kuvuka kila aina ya kikwazo, kuinuka kila unapoanguka na kuendelea na mapambano kama vile hakuna kilichotokea.
Ushindi ni matokeo ya kutokukata tamaa na kuendelea na mapambano, kumaliza kila ulichoanza na kuinuka kila unapoanguka. Kama hujapata unachotaka, bado safari haijaisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,