Mara nyingi nimekuwa nakuambia unaposoma hadithi za mafanikio ya wengine zisome kama sehemu ya kupata hamasa kwamba inawezekana, lakini siyo kwa ajili ya kuiga kile ambacho wao wamefanya.
Kwa sababu hata wao wenyewe kama wangeanza tena sasa, na wakafanya kila walichofanya kwa namna walivyofanya kipindi cha nyuma, hawatafanikiwa kama walivyofanikiwa huko nyuma.
Na hii ni kwa sababu kuu moja; hakuna anayejua anachofanya. Hii ni kauli ambayo nimewahi kukuambia tena, lakini leo nataka nikukumbushe ili iweze kukukaa vizuri na uweze kufanya maamuzi sahihi kwako.
Unaweza kuona watu wanaweka malengo makubwa na kuyafikia, ukafikiri wana njia ya uhakika wanayojua wataitumia kufikia malengo yao. Lakini hiyo siyo kweli, watu wanaweza kuweka malengo makubwa, lakini njia ya uhakika ya kufikia malengo hayo hawana.
Badala yake wanaangalia pale walipo, na kujiuliza hatua zipi sahihi kuchukua na wanachukua hizo, huku wakiangalia kule wanakokwenda. Hakuna yeyote mwenye uhakika wa kesho, hakuna mwenye uhakika wa matokeo ya kile anachofanya, ila watu wanafanya kwa sababu ndiyo kitu sahihi.
Katika kufanya huko, mara nyingi wanapata matokeo ambayo siyo sahihi au waliyotaka, lakini hawajali hilo, badala yake wanajifunza na kuchukua hatua nyingine bora zaidi. Wanaenda hivyo mpaka wanapopata kile wanachotaka.
Kwa kujua hili linakusaidia mambo mawili;
Moja ni kuanza kufanya hata kama bado hujawa na uhakika. Wengi huahirisha kuanza wakisubiri kupata uhakika, hakuna wakati unaweza kuwa na uhakika wa kila kitu, hivyo ni bora kuanza kuliko kuendelea kusubiri.
Mbili ni kufanya chochote kuliko kutokufanya kabisa. Unapokuwa njia panda na hujui nini ufanye, ni bora ukafanya chochote kuliko kutokufanya kabisa. Unapofanya chochote na ukakosea, unakuwa na nafasi ya kurekebisha, maana umejifunza. Lakini usipofanya kabisa, huna hata cha kurekebisha, kwa sababu hakuna ulichojifunza.
Usisubiri mpaka uwe na uhakika ndiyo ufanye, hakuna mwenye uhakika. Tathmini pale ulipo sasa, chukua hatua, pata matokeo, yatathmini kisha fanya kwa ubora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,