Kama unataka kuibadili dunia, nenda nyumbani ukaipende familia yako, hii ni kauli ambayo iliwahi kutolewa na Mama Theresa.
Ni kauli fupi lakini iliyobeba ujumbe mkubwa, siyo tu kwenye maisha, bali kwa upande wa mafanikio pia.
Moja ya vikwazo vinavyotuzuia kufanikiwa ni kuhangaika na mambo makubwa ambayo yako nje kabisa ya uwezo wetu, huku tukiacha mambo madogo tunayoweza kufanya na yakawa na manufaa.
Unahangaika na mambo makubwa, mambo ambayo yanakupa hamasa na kukusisimua kweli, lakini hakuna hatua unazoweza kuchukua kufikia mambo hayo makubwa.
Kujiwekea malengo makubwa ni hitaji muhimu kwenye mafanikio, kuwa na maono na ndoto kubwa unayotaka kufikia kwenye maisha yako ni jambo zuri.
Lakini katika kuchukua hatua, maono na ndoto hizo kubwa zinaweza kuwa ganzi kwako, usijue wapi pa kuanzia.
Na hapa ndipo unapopaswa kuwa na hatua ndogo unazoweza kuchukua kila siku na baadaye zikakufikisha kwenye maono yako makubwa.
Kwa kila maono na ndoto kubwa ulizonazo, gawa kwenye hatua ndogo ndogo za kuchukua kila siku. Kisha kila unapoianza siku yako, kazana na kukamilisha hatua za siku hiyo.
Usisumbuke na kile kikubwa unachotaka kufikia, wewe sumbuka na kile unachopaswa kufanya leo. Na pale unapokutana na vikwazo na kutaka kukata tamaa, angalia kule unakokwenda ili kupata hamasa zaidi.
Ukitaka kupanda mlima mrefu, hulali na kuamka ukajikuta kwenye kilele cha mlima, badala yake unapiga hatua moja baada ya nyingine, na hatua ya mwisho inakufikisha kwenye kilele.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio, hakuna kitu kimoja utakachofanya kikakutoa ulipo sasa na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. Bali zile hatua unazochukua kila siku zinajijenga na mwisho kuwa mafanikio makubwa.
Kwa chochote unachofanya, kigawe mpaka ufike kwenye hatua za kuchukua kila siku, kisha jenga nidhamu ya kuchukua hatua hizo.
Ni biashara, una maono ya kuikuza iwe kubwa na inayojiendesha yenyewe. Njia ya uhakika ya kufika huko ni kutoa huduma bora kwa wateja wako ili waweze kurudi tena, huku ukiendelea kuwafikia wateja wengi zaidi. Hayo ndiyo mambo ya kufanyia kazi kila siku, kuwahudumia vizuri wateja ulionao sasa na kutafuta wateja wapya. Pia kuhakikisha sehemu ya faida inarudi kwenye biashara ili kukua mtaji na biashara kwa ujumla.
Ni kazi, igawe mpaka ufikie kile unachopaswa kufanya kila siku. Kwenye uandishi, gawa mpaka upate maneno ya kuandika kila siku.
Acha kusumbuka na mambo makubwa na jipe namba yako ya kufanyia kazi kila siku, kisha ifanyie kazi namba hiyo.
Unachohitaji ni nidhamu ya kuhakikisha kila siku unachukua hatua ulizopanga kuchukua. Kwa kujijengea nidhamu hiyo na kuchukua hatua hizo, mafanikio utakutana nayo kadiri unavyokwenda, kama tu hutaiacha njia yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,