Kila kiumbe hai anakuja duniani akiwa na njia mbalimbali za kumkinga na hatari atakazokabiliana nazo kwenye mazingira yake.
Simba wana meno makali na nguvu za kuweza kupata chakula chao na pia kujikinga na maadui.
Swala wana masikio yenye kunasa haraka na mbio kali za kuwawezesha kukimbia hatari ya simba.
Ndege wana mabawa, manyoya na miili iliyoundwa kwa namba ambayo wanaweza kuruka angani.
Samaki wana mapezi na aina ya miili inayowawezesha kuishi kwenye maji.
Mnyama asiyetumia na kuendeleza uwezo aliozaliwa nao, haishi maisha marefu.
Swali ni je, binadamu tuna nini cha kutuwezesha kujikinga na hatari mbalimbali za maisha?
Sisi binadamu tuna uwezo wa kuwatawala viumbe wengine japo hatuna nguvu kama walizonazo wao, ila tuna kitu kimoja ambacho viumbe wengine hawana.
Kitu hicho ni uwezo wa kufikiri. Viumbe wengine wote wanazaliwa wakiwa na mpangilio wa maisha yao, hivyo wanaenda kama ilivyopangwa. Lakini sisi binadamu tuna uwezo wa kufikiri kwa kila tunachokabiliana nacho na kufanya maamuzi sahihi.
Binadamu yeyote anayekabiliana na changamoto mbalimbali kwenye maisha, anayekutana na hatari na zikamdhuru, ni kwa sababu hajatumia au kuendeleza uwezo wa kufikiri uliopo ndani yake.
Hii imekuwa tabia ya walio wengi, badala ya kufikiri na kufikia maamuzi yao wenyewe, wanafuata kundi linafanya maamuzi gani. Hivyo inapotokea kundi linaongozwa na mtu asiyeweza kufanya maamuzi sahihi, wote wanaangamia.
Wale wanaotaka kuwashawishi watu wafanye maamuzi fulani yatakayowanufaisha, iwe ni wanasiasa wanaotaka kuchaguliwa, watu wa mauzo wanataka kuuza walichonacho au matapeli wanaotaka kujipatia vitu kwa ulaghai, wanahakikisha yule wanayetaka kumshawishi hafikiri.
Kwa sababu fikra ndiyo silaha pekee ambayo mwanadamu anayo ya kukabiliana na kila hatari na changamoto, ukitaka kumshinda, hakikisha hafikiri. Hebu pata picha uko porini na unakutana na simba ambaye hana meno wala kucha, hutajisumbua hata kukimbia, na kama unapenda nyama ya simba, siku hiyo unakuwa umepata kitoweo rahisi.
Rafiki, ninachotaka kukuambia hapa ni kimoja, kwa kila maamuzi unayoyafanya, hakikisha umefikiri wewe mwenyewe kwa kina na kufikia maamuzi hayo.
Kwa kila maamuzi ambayo watu wanakulazimisha ufanye haraka kwa sababu ukichelewa utapitwa, au unasisitizwa wengine wote wanafanya hivyo kasoro wewe, au unaambiwa kuna uhaba au mwisho, kataa kuyafanya.
Jipe muda kwanza wa kuyatafakari, kuangalia kila upande ndipo ufikie maamuzi yako mwenyewe. Na hakikisha haiwi siku hiyo hiyo, kwa sababu wengi wana ushawishi mkali, ambapo unahitaji muda ushawishi wao ufutike kwenye mawazo yako ndiyo uweze kufikiri kwa usahihi.
Tumia akili yako kunusa hatari na epuka kufanya maamuzi ambayo yatakugharimu baadaye.
Kujiwekea baadhi ya sheria na misingi utakayokuwa unaisimamia itakusaidia sana kuepuka kufanya maamuzi yatakayokugharimu.
Baadhi ya sheria na kanuni zinazoweza kukusaidia;
- Sitafanya maamuzi yoyote nikiwa na hasira sana au furaha sana, nitasubiri mpaka hisia hizo zitulie ndiyo nifanye maamuzi.
- Sitafanya maamuzi ya kununua kitu pale ninaposikia kauli hizi; punguzo la bei ni leo tu… bidhaa/nafasi ni chache, wahi sasa… kila mtu anayo, umebaki wewe tu… wajanja wote wana hii….
- Chochote ambacho naambiwa kina faida kubwa, hatari ndogo na hakihitaji kuweka kazi sitajihusisha nacho.
- Njia yoyote ya mkato ya kupata kitu chenye thamani siyo njia sahihi.
- Kila kinachotokea kimesababishwa, ninapoona matokeo nitaangalia kilichosababisha kwanza.
- Nikiona watu wananing’ang’aniza sana kuingia kwenye fursa fulani, basi mimi ndiyo fursa kwao.
Hizi ni baadhi, endelea kuongeza zako ambazo zitakusaidia kwenye kufanya maamuzi mbalimbali.
Kwa kanuni za aina hii, kuna baadhi ya fursa utazikosa, lakini zitakusaidia kuepuka kila aina ya fursa mbaya, na hivyo utakuwa kwenye nafasi ya kupata fursa ambazo ni kubwa kuliko zile unazopoteza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,