“Any fool can criticize, condemn and complain—and most fools do.
But it takes character and self-control to be understanding and forgiving.” – Dale Carnegie
Ukitaka kurahisisha maisha yako, angalia wengi wanafanya nini kisha usifanye kama wao.
Hii ni kwa sababu wengi huwa hawafanyi kilicho sahihi, bali wanafanya kilichozoeleka.
Kuna sumu tatu zinazoathiri mahusiano ya kila aina.
Sumu hizi zina madhara makubwa, ila wengi hawayaoni na kuziepuka.
Sumu hizo ni kukosoa, kuhukumu na kulalamika.
Ni rahisi kukosoa kile ambacho mtu amefanya, bila hata ya kukijua kwa undani.
Ni rahisi kuhukumu wengine kwa kile unachoona kwa nje.
Ni rahisi kulalamika pale mambo yanapokwenda tofauti na matarajio yako.
Lakini yote hayo hayajawahi kuwa na matokeo mazuri.
Wanaokosolewa huwa wanazidi kuamini kwenye kile walichokosolewa.
Wanaohukumiwa huwa wanazidi kusisitiza wako sahihi.
Na wanaolalamikiwa huwa wanaonesha hawana hatia.
Ili kujenga mahusiano bora na kuwa na ushawishi mzuri kwa wengine,
Tunapaswa kuepuka sumu hizo tatu,
Na tunapaswa kuwaelewa watu, kujua kile wanachopitia, kujiweka kwenye nafasi zao na kisha kuwasamehe.
Wasaidie watu kuona kipi sahihi na bora zaidi kwao kufanya na wataona na kufanya.
Walazimishe watu kipi wanapaswa kufanya na watakupinga, hata kama ni kitu chenye manufaa kwao.
Kumbuka binadamu ni viumbe wa hisia,
Ukitaka kuingia kwenye mioyo yao, kamata hisia zao.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu jawabu la karibu changamoto zako zote za maisha, fungua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/08/01/2040
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani.