Mafanikio ya haraka, ambayo pia humfanya mtu kuwa maarufu kwa muda mrefu, huwa yanatokana na bahati fulani ambayo mtu amekutana nayo.
Lakini kwa kuwa sisi binadamu huwa tunapenda hadithi, na bahati haitengenezi hadithi nzuri, basi watu hutengeneza hadithi nyingine inayovutia kwenye mafanikio hayo ya haraka.
Inaweza kuwa hadithi inayoeleweka vizuri, lakini siyo ukweli. Hivyo watu huamini hadithi hizo, na ghafla wanaanza kuchukua maamuzi ambayo siyo sahihi.
Wanafikiri kuna ambacho wamefanya ambacho kimewapa mafanikio waliyopata, hivyo wanaendelea kufanya baadhi ya vitu hivyo na siyo tu haviwafikishi kwenye mafanikio, bali vinakuwa chanzo cha wao kuanguka.
Kwa kutambua hili, unapaswa kuwa makini sana na mafanikio ya haraka, unapaswa kujua wazi wapi bahati imekuendea vizuri na usipate kiburi kufikiri unajua kila kitu.
Wengine wanaweza kukusifu kwa makubwa uliyofanya, lakini usidanganyike wala kulewa sifa hizo. Tambua ndani yako ukomo wa uwezo na mchango wako na sehemu ya bahati. Kisha epuka kabisa kufanya chochote kilicho nje ya uwezo wako, hata kama watu wataamini una uwezo zaidi ya huo.
Ni kanuni ya asili kwamba kila kiendacho juu hushuka chini, na kile kinachopanda haraka na kwenda juu zaidi, huanguka haraka na kwa kishindo kikubwa.
Tumekuwa tunaona hili kwenye maisha ya wengi, anakutana na bahati fulani ambayo inampa mafanikio makubwa, anafikiri ni kitu fulani alichofanya, anarudia kufanya na anaanguka vibaya.
Sisemi usitambue mchango wa juhudi na uwezo wako, sisemi usitegemee misingi unayoifanyia kazi, ila ninachosema ni hiki, jua ni wakati gani mafanikio yamekuja kwa juhudi zako na jua wakati gani yamekuja kwa bahati.
Kadiri bahati inavyokuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yako, ndivyo unavyopaswa kuwa makini, maana hapo kuna hatari ya kufanya mambo yatakayoharibu mafanikio yako kwa haraka.
Hili pia litumie wakati unajifunza kwenye mafanikio ya wengine, usiangalie wale waliopata mafanikio ya haraka na ambao ni maarufu, bali angalia wale ambao wamepata mafanikio na kukaa nayo kwa muda mrefu. Hao kuna kitu wanafanya ambacho kinajenga na kulinda mafanikio yao. Wakati wale wanaopata mafanikio ya haraka na umaarufu wa ghafla, miaka michache baadaye hutawasikia tena.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kocha, kuna mchango wa bahati, pia kuna mchango wa juhudi. Na kwenye juhudi kuna ukomo. Ubarikiwe kwa makala hii nzuri.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike