Kuna vitu unaweza kufanya sasa na usione madhara yake, lakini baadaye vinakuja kuwa kikwazo kikubwa kwako.
Hivyo kwa kila unachotaka kufanya, angalia kwanza mbeleni kitakuathiri kiasi gani, angalia miaka 10, 20 mpaka 50 ijayo kisha ona kitakuwa na athari gani.
Mambo mengi yanayokukwamisha sasa, ni matokeo ya kile ulichofanya kipindi cha nyuma.
Chukua mfano wa madeni, wakati wa kukopa, huwa huangalii madhara ya mbeleni. Lakini baada ya kutumia mkopo uliochukua, ndipo unakuja kugundua kwamba ulijiweka kwenye shimo ambalo linakunyima uhuru mkubwa.
Kama ulichukua mkopo wa muda mrefu na ukafanya kitu, baadaye hutaona sana kile ulichofanya, bali utaona uzito wa deni ulilonalo. Deni hilo litakunyima uhuru wa kufanya mambo yako kwa sababu itabidi ufanye kazi ili kulipa deni.
Hata kama kuna fursa nyingine nzuri zaidi kwako hutaweza kuifanyia kazi, kwa sababu umenasa kwenye deni hilo.
Mbaya zaidi ni pale deni hilo linapofanya kipato chako kuwa kidogo, hivyo kulazimika kuendelea kuchukua mikopo ili kufidia kipato unachokosa. Hilo linazidi kuchimba shimo linalokunyima uhuru zaidi na zaidi.
Huo ni mfano mmoja kwenye fedha, hasa upande wa madeni. Mifano ni mingi, kuanzia kwenye mahusiano, misaada unayopewa, zawadi mbalimbali. Kuna vitu utavipokea au kuvikubali sasa, kwa kuwa huoni madhara yake sasa, lakini siku zijazo kinakuja kuwa kikwazo kwako kufanya mambo yako.
Hivyo wajibu wako mkubwa ni kulinda uhuru wako, kwa kila unachofanya, angalia kinaathirije uhuru wako kwa siku zijazo. Unapaswa kuwa huru wakati wowote, kuchukua hatua ambazo zina manufaa kwako.
Usiuze kesho yako kwa sababu ya njaa uliyonayo leo, hujui kesho inakuja na nini, hivyo fanya kila unachoweza kufanya leo, ili uivuke leo ukiwa hai, huku ukiwa huru kuikabili kesho kwa namna itakavyokuja kwako.
Mafanikio ya kweli ni uhuru, ulinde kwa gharama yoyote ile.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante huu ukurasa umesheheni maarifa sana
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike