“If you could only know who you are, all your troubles would seem utterly unnecessary and trivial.” – Leo Tolstoy
Sehemu kubwa ya matatizo ambayo unapitia kwenye maisha, yanatokana na mtu kutokujijua wewe mwenyewe.
Unahangaika na mambo mengi kwa sababu hujajijua kwa undani.
Unafuata kila ambacho wengine wanakuambia lakini bado ndani yako hupati ridhiko.
Jamii inakuambia unapaswa kuwa hivi au vile, na wewe unakuwa kama unavyoambiwa, na matatizo ndiyo yanazidi.
Unawaangalia wale waliofanikiwa na kujiambia unataka kuwa kama wao, unapambana na kuwafikia, lakini bado ndani yako hakuna utulivu.
Huwezi kupata utulivu na matatizo yako hayataisha kama utaendelea kuishi maisha ya wengine.
Njia ya uhakika ya kumaliza sehemu kubwa ya matatizo unayokutana nayo kwenye maisha ni kujijua wewe mwenyewe kiundani, kujitambua.
Ukishajitambua, ishi kwa namna yako ya kipekee.
Unapowaona wale waliofanikiwa, usikazane kuwa kama wao, bali watumie kama hamasa ya wewe kuwa wewe.
Maana wale waliofanikiwa kweli, ukiwaangalia utagundua wamechagua kuyaishi maisha yao.
Njia pekee ya kujitambua ni kujisikiliza mwenyewe,
Kuachana na kelele za dunia na kuangalia ndani yako.
Kuangalia yale umekuwa unafanya na yapi unapendelea zaidi.
Na kujua kipi hasa kinachokusukuma na kukupa matumaini.
Zama tunazoishi ni zama zinazowapoteza wengi,
Kelele ni nyingi, washauri ni wengi,
Lakini mtu pekee anayekujua wewe kwa undani, ni wewe mwenyewe.
Hivyo usimsikilize yeyote anayekuambia mafanikio ni kuwa namna fulani tu au kufanya kitu fulani tu.
Unachopaswa ni kuiishi misingi sahihi na kisha kupambana kuwa wewe, na siyo kuwaiga wengine.
Misingi haikubani au kukunyima kuwa wewe, bali inakupa mwongozo na kukuweka huru kuwa wewe.
Jitambue na shika hatamu ya maisha yako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu muda na pesa kama njia nzuri ya kupima vipaumbele vyako na kuona kule unakokwenda, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/08/26/2065
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.