Mbinu zote za mafanikio ya haraka ambazo watu wamekuwa wanajifunza zimekuwa hazifanyi kazi kwao kwa sababu zinaondoa kiungo kimoja muhimu, kazi.
Hakuna mafanikio ambayo hayahitaji kazi, kufikia mafanikio makubwa kwa haraka bila ya kuweka kazi ni kitu ambacho hakipo. Hivyo usije ukadanganyika hata kidogo.
Kama unachotaka ni kupata mafanikio ya haraka, na hapa haimaanishi kwa muda mfupi, bali kwa muda ambao ni mfupi ukilinganisha na kupita njia ya kawaida, basi mbinu ziko nne za kufanyia kazi.
Mbinu ya kwanza ni kupata mrejesho wa haraka kwa yale unayofanyia kazi. Iwe ni kitu unachozalisha au mazoezi unayofanya, unahitaji kupata mrejesho kutoka kwa wale wanaoguswa na unachofanya. Mrejesho huo unakuonesha maeneo ambayo una udhaifu na kuweza kuyafanyia kazi mapema na kuwa bora. Kama hupati mrejesho wa kweli, utaendelea kufanya kisichokupa matokeo.
Mbinu ya pili punguza na ondoa kabisa kila aina ya usumbufu. Chochote ambacho hakiendani na kule unakotaka kufika ni usumbufu. Muda wowote unaopeleka kwenye usumbufu huo ni muda ambao unajipunja kwenye kufanya makubwa. Hivyo njia hapa ni kujua kile unachotaka, unachopaswa kufanya ili kukipata na kisha kupuuza mengine yote ambayo hayana mchango wa kukufikisha unakotaka kufika.
Mbinu ya tatu ni kuzungukwa na mazingira yanayokusukuma kuwa bora zaidi. Mazingira yana nguvu ya kukusukuma kufanya zaidi au kukurudisha nyuma usifanye. Mazingira ni pamoja na wale wanaokuzunguka, upatikanaji wa vitu unavyohitaji na uwepo wa wale wanaohitaji unachofanya. Tengeneza mazingira yatakayokulazimisha wewe ufanye makubwa na siyo kuridhika na madogo.
Mbinu ya nne ni kucheza mchezo ambao unatumia uwezo ulio ndani yako. Kama unakazana kujibadilisha au kuiga wengine jua una kazi mbili mbele yako, kazi ya kubadilika ni ngumu na huwa haizai matunda. Hivyo badala ya kubadilika uwe kama fulani, chagua kuwa wewe. Fanya kile kinachoendana na uwezo ulio ndani yako, kinachotumia vipaji ulivyo navyo. Wakati wengine wataona ni kazi, wewe utaona ni mchezo na hivyo utakuwa tayari kufanya zaidi.
Tumia mbinu hizo nne kwa pamoja, na kile ambacho kingekuchukua miaka 20 kufikia, kitakuchukua miaka 10. Utafanya ukiwa na uhakika na siyo kwa kubahatisha. Na mafanikio yatakuwa yako, ndani ya muda ambao wengi watashangaa.
Kuvunja na kutokujali mbinu hizo nne imekuwa chanzo cha wengi kushindwa kufanya makubwa kwenye maisha yao, hivyo wewe ukizizingatia, hata kama haitakuwa ndani ya muda mfupi, jua kwa hakika utafanya makubwa, ni swala la muda tu, hivyo kuongeza uvumilivu itakusaidia zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,