“There are people who make no mistakes because they never wish to do anything worth doing.” – Johann Wolfgang von Goethe
Kuna watu ambao wamekuwa wanafikiri kwamba kama hawakosei basi ni wakamilifu, kama hakuna wanaowapinga na kuwakosea basi wanafanya kilicho sahihi.
Lakini huko ni kujidanganya.
Ukweli ni huu;
Kama hukosei maana yake hakuna kikubwa unachofanya kwenye maisha yako.
Kama hupingwi na kukosolewa, hakuna kitu cha tofauti unachosimamia kwenye maisha yako.
Kama unafanya kile ambacho umezoea kufanya kila siku, utaendelea kupata matokeo ambayo umezoea kupata na hutakosea, lakini pia hutapata matokeo makubwa na ya tofauti.
Kama unaishi kama wengine wanavyoishi na hakuna msimamo wowote wa tofauti ulionao, utapata matokeo kama ambayo wengine wanayapata na hakuna atakayekupinga au kukukosoa, lakini pia hutafanya makubwa.
Utakapoanza kufanya mambo makubwa na ya tofauti na ulivyozoea, utakosea. Makosa hayo yatakuwa sehemu ya kujifunza ili uwe bora zaidi.
Hivyo usijisifie kwamba hukosei, bali jiulize ni yapi ya tofauti unayofanya?
Utakapochagua kuyaishi maisha yako na kuacha kufuata mkumbo, utavutia kila aina ya wapingaji na wakosoaji, unapowaona hao wakija kwako, siyo kwamba umekosea, bali umekuwa tofauti.
Usijisifie kwa kutokupingwa au kukosolewa, bali jiulize ni kipi cha tofauti unachosimamia kwenye maisha yako.
Kukosea, kukutana na magumu na changamoto na kupingwa pamoja na kukosolewa ni ishara nzuri kwamba unafanya vitu vya tofauti na hivyo ndivyo vyenye fursa ya wewe kufanikiwa zaidi ya pale ulipo sasa.
Ogopa sana pale mambo yanapokwenda kimtelezo, unakuwa kwenye njia isiyo sahihi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kuchagua kufa, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/30/2100
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.