Fikiria upo kwenye biashara na umefika hatua ambayo badala wewe uwabembeleze wateja wanunue, wateja wanakubembeleza wewe upokee pesa zao, ukubali kuwauzia kile unachouza.

Unafikiri hizo ni ndoto? Ni uhalisia kabisa, biashara zote ambazo zimeweza kufikia mafanikio makubwa, zimeweza kufika hatua hiyo ya wateja kubembeleza kuuziwa, wateja wanaiomba biashara ipokee pesa zao na kuwauzia kile ambacho biashara inauza.

Mifano ipo mingi, lakini tutumie mfano mmoja ambao ni maarufu na umekuwa unajirudia kila mwaka. Kampuni ya Apple ambayo inatengeneza simu ya Iphone, huwa inakuja na toleo jipya la simu hiyo karibu kila mwaka. Inapofika siku ya mauzo ya toleo jipya, watu hujipanga mstari na kukesha kwenye maduka ili kuwa wa kwanza kupata toleo jipya la simu.

Siyo kwamba simu hizo zinatolewa bure, zinauzwa, tena ghali sana. Na siyo kwamba mauzo ya simu hiyo ni kwa siku moja tu, zinaendelea kupatikana milele, lakini watu wapo radhi kwenda kukesha, ili kuwa wa kwanza kupata toleo jipya.

Hali hiyo haijatokea kama ajali, bali imetengenezwa na kampuni hiyo kwa muda mrefu, kuwageuza wateja kuwa waumini wa biashara yao, kuacha kujiona kama wateja na kujiona kama sehemu ya biashara. Kuna njia nyingi za kuweza kutengeneza hilo, ambazo hata wewe unaweza kuzitumia na kuigeuza biashara yako kuwa ya wateja kukubembeleza kununua.

Kitu cha kwanza na kikubwa unachopaswa kufanya kwenye biashara yako ni kutoa thamani kubwa ambayo mteja hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile. Toa kitu ambacho hakuna mshindani anaweza kufanya hivyo, mfanye mteja awe hana pengine pa kupata unachotoa ila wewe, na maisha yake hayawezi kukamilika bila kupata kile unachotoa.

Unaweza kuona hilo ni gumu, hasa ukizingatia namna watu wanaingia na kuendesha biashara zao. Lakini nikuhakikishie kitu kimoja, biashara yoyote ile unayoifanya, ukiifanya kama wewe, ukaweka utu wako kwenye biashara hiyo, lazima utatoa kitu ambacho hakuna mwingine anayeweza kukitoa, hivyo kuwa wewe na toa thamani kubwa kwa wateja wako.

Kitu cha pili unachopaswa kukifanya ili biashara yako iweze kuwa na wateja wanaokubembeleza uwauzie ni kuwa na msimamo na kutegemeka. Pale unapowaahidi wateja kitu fulani, basi wanakipata kweli. Huduma unazotoa ni bora wakati wote, thamani unayozalisha ni ya juu wakati wote, mteja hana wasiwasi anapokuja kwako, kwa sababu anajua anakuja kupata kilicho bora.

Hili pia siyo gumu kufanya, kama utaweka umakini mkubwa kwenye biashara yako, ukaijua nje ndani na kuhakikisha unatekeleza kile ulichoahidi.

Kitu cha tatu muhimu kufanya ni kuzijua silaha za ushawishi za kisaikolojia, ambazo zinawafanya wateja wakuamini na kuiamini biashara bila ya kufikiria mara mbili. Hizi ni silaha ambazo ukiwa nazo na ukizitumia vizuri, biashara yako itanufaika sana.

Robert Cialdini kwenye kitabu chake kinachoitwa Influence ametushirikisha silaha sita za ushawishi ambazo pia nakwenda kukushirikisha hapa na jinsi ya kuzitumia kupata wateja waaminifu na watakaokubembeleza uwauzie.

Silaha ya kwanza ni KULIPA FADHILA, hapa unapaswa kuanza kuwapa thamani kubwa wateja wako kabla hata hawajakulipa, kiasi kwamba unapowaambia kuna kitu unauza, mara moja wanakinunua. Ndani yao wanakuwa na deni la kukulipa kutokana na thamani kubwa uliyoanza kuwapa bure kabisa.

Silaha ya pili ni DHAMIRA NA MSIMAMO, hapa unapaswa kuwafanya wateja wako waweke dhamira na kufanya maamuzi fulani yanayohusu biashara yako na baadaye watahakikisha wanalinda msimamo wao kwa kuendelea kutunza kile walichoamua. Mfani mtu akinunua mara moja ni rahisi kununua tena.

Silaha ya tatu ni KUFUATA MKUMBI, hapa unapaswa kuwafanya wateja wako waone wapo ndani ya kundi la watu ambao wanafanya maamuzi kama yao, hivyo jenga sifa fulani ya biashara yako na ambayo inavutia wateja wenye sifa fulani, baada ya hapo wateja wenye sifa ile watafuata mkumbo, kwa kuja kwa sababu wanaofanana nao wako kwenye biashara yako.

Silaha ya nne ni MAMLAKA, hapa unapaswa kujijengea mamlaka fulani kupitia biashara yako au kutumia mamlaka zinazohusika na biashara yako kuwafanya wateja waiamini. Watu wana tabia ya kuamini mamlaka kwa sababu zinajua, hivyo jijengee wewe na biashara yako mamlaka fulani, inaweza kuwa ubobezi kwenye kile mnachouza na hapo wateja watakuwa na imani zaidi.

Silaha ya tano ni KUPENDA, wafanye wateja waipende biashara yako kwa namna ilivyopangiliwa na wale waliopo kwenye biashara hiyo. Hakikisha kila aliye kwenye biashara anakuwa nadhifu na anayevutia kwa wateja. Pia hadhi ya eneo la biashara inapaswa kuwa ya juu, kitu kinachowafanya wateja waipende zaidi.

Silaha ya sita ni UHABA, hapa unapaswa kutengeneza uhaba unaowasukuma watu kuchukua hatua fulani. Bila uhaba watu huwa hawasukumwi kuchukua hatua, hivyo unaweza kuwa na ofa yenye ukomo au idadi ya bidhaa au nafasi za huduma zenye ukomo na kisha kuwaeleza wazi wateja wako. Kwa kuona uhaba uliopo, watasukumwa kuchukua hatua.

Angalizo, silaha hizo sita unaweza kuzitumia kwa uongo na ukawahadaa wateja wako, lakini hilo litakuwa kikwazo kwako baadaye kwa sababu utajijengea sifa mbaya. Zitumie silaha hizo sita kwa ukweli na uaminifu na wateja ataiamini biashara yako kwa kuwa tayari kukubembeleza uwauzie.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha