Kufanya tahajudi ni moja ya njia za kutuliza fikra zako na kupata utulivu kwenye dunia ya sasa ambayo ina usumbufu wa kila aina.
Zipo aina nyingi za tahajudi, ambazo zina mbinu mbalimbali za kufanya. Wengi wamekuwa wanasema hawawezi kufanya tahajudi kwa kuwa hawana muda au utulivu wa kufanya baadhi ya tahajudi.
Kwa wale ambao hawawezi kufanya tahajudi kwa mbinu zinazofundishwa, kuna njia ya kunufaika na matokeo ya tahajudi, kwa kuchagua kufanya kila kitu kama tahajudi.
Kwa kila kitu unachochagua kufanya, unaweza kukitumia kama njia ya wewe kufanya tahajudi na ukanufaika sana.
Unachofanya ni kupeleka mawazo yako yote kwenye kitu hicho unachofanya. Wakati unapofanya kitu hicho, sahau mambo ya nyuma, sahau yajayo na achana na hofu au wasiwasi wowote ulionao. Wewe weka fikra zako na umakini wako wote kwenye kile unachofanya, kile tu kilicho mbele yako.
Kwa kufanya kitu hivi, utafanya kwa umakini mkubwa, ufanisi utakuwa juu na utazalisha matokeo mazuri, lakini pia utakuwa na utulivu mkubwa.
Kinachowafanya wengi kuchoka ni kufanya kitu kimoja huku mawazo yakiwa sehemu nyingine tofauti kabisa. Ondokana na hali hiyo ya kwa kufanya kila kitu kuwa tahajudi.
Hata kama unakula, peleka umakini wako wote kwenye zoezi la kula, unapotafuta, weka umakini wako kwenye kutafuna, isikie ladha ya chakula, meza na kisikia chakula kikishika kwenye koo lako kwenda tumboni. Kwa kufanya hivi utanufaika mno na zoezi dogo la kula, kuliko unapokula huku mawazo yako yakizurura maeneo mengine.
Wote tunajua jinsi ambavyo tunapokuwa na jambo muhimu kufanya na muda mfupi wa kufanya tunavyoweka umakini wetu wote kwenye jambo hilo. Kumbe tayari uwezo wa kufanya kitu kama tahajudi tunao, tumekuwa tu hatuutumii mara kwa mara.
Anza sasa kutumia uwezo huo, kwa kugeuza kila unachofanya kama tahajudi, utafanya makubwa huku ukiwa na utulivu mzuri. Kila unachochagua kufanya, kichukulie ni kitu muhimu kuliko vingine vyote kwa muda huo, chukulia kama kitu cha mwisho kwako kufanya na hivyo weka umakini wako wote kwenye kitu hicho, manufaa utakayoyapata ni makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha.
LikeLike
Karibu Datius.
LikeLike